Saturday, October 13, 2012

MESSI: SIKUOTA KUTWAA TUZO ZOTE NILIZOPATA... SASA KILICHOBAKI NI KOMBE LA DUNIA TU

Messi akiwa uwanjani. Mkali huyo usiku wa kuamkia leo alifunga magoli mawili na kuisaidia Argentina kushinda 3-0 dhidi ya Uruguay.

LIONEL Messi amesema hakuwahi kuota kama angekuja kutwaa tuzo zote alizopata, na amesisitiza kwamba "kitu pekee kilichobaki ni Kombe la Dunia" ili kukamilisha maisha yake ya soka ya kimafanikio.

"Nini ninachoota sasa? Baada ya yote niliyotwaa, ni kushinda taji na Argentina, kwenye Kombe la Dunia. Nimepata mataji karibu yote, kwa ngazi binafsi na ngazi ya klabu, na hiki ndicho kitu kimoja ninachokikosa," straika huyo wa Barcelona aliiambia televisheni ya C5N.

"Hata katika ndoto zangu za kiwazimu sikuwahi kuota kama ningekuja kutokewa na haya yaliyonitokea. Lakini hili ndilo taji pekee ninaloli-miss", straika huyo mwenye umri wa miaka 25 alisema kuelekea mechi yao ya Argentina dhidi ya Uruguay katika hatua ya mtoano ya Kombe la Dunia 2014 Kanda ya Amerika Kusini ambayo walishinda 3-0 usiku wa kuamkia leo ambapo Messi alifunga magoli mawili na Sergio Aguero kuongeza moja.

Pia alisema mahusiano yake ya sasa na mashabiki wa nyumbani kwao ndivyo alivyotaka yawe. "Daima nilidhamiria iwe hivi, mambo yaende vyema, na pia nipendwe na watu wa nyumbani kwangu na wengine kutoka mahala kwingine. Lakini nilikuwa nikija hapa mambo yalikuwa ni tofauti na kwingineko nilikokuwa nikienda. Hivi sasa jambo hilo limebadilika na hilo linanipa furaha sana. Matokeo yanaleta mengi sana. Unaposhinda, mambo hubadilika," aliongeza.

"Tunafahamu kwamba tuna safari ndefu sana ya kwenda ili kuwa timu kali, lakini ipo fursa kubwa kwetu kukua," alisema.

No comments:

Post a Comment