Sunday, October 21, 2012

SIMBA AKWAMA KWENYE BUTI LA MGAMBO

Straika wa Simba, Felix Mumba Sunzu akivaa soksi baada ya kurudishwa benchini na refa Othman Lazi wa Morogoro ili akavae sawa na wachezaji wenzake kabla ya kuanza kwa mechi yao ya Ligi Kuu ya Vodacom dhidi ya Mgambo JKT kwenye Uwanja wa Mkwakwani Tanga leo. Jambo hilo lilimfanya achelewe kupiga picha na wachezaji wenzake wa kikosi cha kwanza.
Nahodha wa Simba, Juma Kaseja (wa nne kulia) akiwalalamikia waamuzi kuhusu kurudishwa benchini kwa straika Felix Sunzu, huku nahodha mwenzake wa Mgambo JKT, Salum Mlima (14) akisalimiana na waamuzi
Wachezaji wa Simba wakiwa katika picha ya pamoja bila ya Sunzu ambaye alirushishwa kwenda kuvaa sawa na wenzake.

Wachezaji wa Mgambo JKT wakiwa katika picha ya pamoja.
Benchi la Simba
Mashabiki wa Simba wakishangilia baada ya timu yao kuingia uwanjani kabla ya kuanza kwa mechi yao dhidi ya Mgambo JKT kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga leo

UWANJA wa Mkwakwani unaonekana si mwepesi kwa Simba baada ya mabingwa hao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kuacha jumla ya pointi nne katika mechi mbili kufuatia kushikiliwa katika sare ya 0-0 dhidi ya Mgambo JKT ya mjini Tanga.

Sare ya nne ya Simba katika mechi tano, imewafanya kufikisha pointi 19, mbili juu ya Azam walio katika nafasi ya pili kwa pointi 17, ambao hata hivyo wamecheza mechi mbili pungufu. Yanga wenye pointi 14 katika nafasi ya tatu, wana mechi moja mkononi.

Kocha msaidizi wa Mgambo, Joseph Lazaro, aliwasifu wachezaji wake baada ya mechi hiyo akisema walifuata maelekezo yake.

"Tuliwaambia wachezaji kwamba kama hawatacheza vizuri watashuka daraja. Hatukupanga kushambulia zaidi ya Simba, tulipanga kucheza kwa kujilinda zaidi ndio maana hatukupata magoli," alisema Lazaro.

Hata hivyo, Mgambo walihitaji bahati pia kuondoka na pointi kwa staili yao ya 'kupaki basi' baada ya mashuti matatu ya wachezaji wa Simba, Mrisho Ngassa (dk.26), Emmanuel Okwi (dk.85) na Felix Sunzu (dk. 89), kugonga mwamba katika matukio ambayo kirahisi Simba wangeweza kupata magoli matatu.    

Kabla ya mechi hiyo mshambuliaji wa Simba, Felix Sunzu, alishindwa kupiga picha na wenzake wa kikosi cha kwanza kutokana na kurudishwa na refa Othman Lazi kutoka Morogoro kwenye benchi lao ili akavae vyema soksi zake ambazo chini zilionekana kuwa na rangi nyingine nyeupe tofauti na wachezaji wenzake.

Katika mechi nyingine za leo, JKT Ruvu imetoka sare ya 1-1 dhidi ya JKT Oljoro kwenye Uwanja wa Chamazi wakati Prisons imeifunga Toto Africans bao 1-0 kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.

Ligi itaendelea Jumatano ambapo Yanga itawakaribisha Polisi Morogoro kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, Azam FC itacheza dhidi ya Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Chamazi,
Coastal Union itawaalika African Lyon (Mkwakwani, Tanga) na Mtibwa Sugar itawakaribisha ndugu zao Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Manungu, Turiani, Morogoro. 

Vikosi vilikuwa;
Simba:

Juma Kaseja, Nassor Said ‘Cholo’, Amir Maftah, Pascal Ochieng, Hassan Hatib, Jonas Mkude, Amri Kiemba/Salim Kinje (dk.88), Mwinyi Kazimoto, Felix Sunzu, Mrisho Ngassa/Edward Christopher (dk.78) na Emmanuel Okwi.

Mgambo JKT:
Godson Massa, Yassin Awadh, Salum Mlima, Bakari Mtama, Salum Kipanga, Ramadhani Maliwa, Chande Magoja/ Nasoro Agumbo (dk.86), Mussa Ngunda, Issa Kandulu, Fully Maganga na Juma Mwinyimvua  

No comments:

Post a Comment