Wednesday, October 24, 2012

SHAKHTAR YAIZAMISHA CHELSEA, BARCA WASHINDA DAKIKA ZA LALA SALAMA, MAN UTD YAZINDUKA

Straika wa Manchester United, Javier Hernandez 'Chicharito' (kulia) akifunga goli dhidi yakipa wa Braga, Beto wakati wa mechi yao ya Kundi H la Ligi ya Klabu Bingwa kwenye Uwanja wa Old Trafford mjini Manchester jana usiku Oktoba 23, 2012. Picha: REUTERS 
LONDON, Uingereza
SHAKHTAR Donetsk waliongoza njia ya timu ndogo baada ya kuwafunga mabingwa watetezi wa Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya Chelsea 2-1 wakati FC Nordsjaelland walikaribia kushinda kwa mara ya kwanza katika michuano hiyo kabla ya kupata sare ya 1-1 dhidi ya Juventus jana usiku.

Barcelona walizinduka kutoka nyuma na wakahitaji goli la dakika ya nne ya majeruhi kuifunga Celtic 2-1 wakati Manchester United walitanguliwa kwa magoli mawili kabla ya kurudisha yote na kuilaza Braga 3-2 kwenye Uwanja wa Old Trafford.

Alex Teixerra aliifungia Shahktar iliyocheza vyema goli la kuongoza mapema katika dakika ya tatu tu mjini Donetsk kabla ya Fernandinho kuongeza la pili kwa timu hiyo ya Ukraine mapema katika kipindi cha pili.

Oscar alifunga la kufutia machozi la Chelsea katika dakika ya 88 wakati klabu hiyo ya London ilipopoteza mechi ya michuano hiyo kwa mara ya kwanza tangu walipotwaa ubingwa huo wa Ulaya Mei.

Ushindi uliwainua Shakhtar hadi kileleni mwa Kundi E wakiwa na pointi saba, tatu juu ya Chelsea ambao wana nne.

Juventus, ambao sasa wametoka sare katika mechi zao zote tisa za Ulaya zilizopita, wana pointi tatu wakati Nordsjaelland wamepata pointi yao ya kwanza katika michuano hiyo.

Nordsjaelland, waliotangulia kwa goli la dakika ya 50 kupitia kwa Mikkel Beckmann, walikuwa wamebakisha dakika tisa tu kupata ushindi wa kukumbukwa wa ugenini kabla ya Mirko Vucinic kuisawazishia Juve katika dakika ya 81.

MANCHESTER UNITED ILIVYOAMKA
Manchester United walifanya kazi nzuri kujiokoa na kipigo cha kufadhaisha kwenye Uwanja wa Old Trafford, waliposhinda 3-2 wakizinduka kutoka 2-0 nyuma kupitia magoli mawili ya Alan ndani ndani ya dakika 20. Walizinduka kwa magoli mawili ya kichwa kutoka kwa Javier Hernandez 'Chicharito' na moja la Jonny Evans.

Ulikuwa ni ushindi wa tatu mfululizo kwa Manchester United na wanaongoza Kundi H wakiwa na pointi tisa, wakifuatiwa na CFR Cluj wenye pointi nne baada ya kutoka sare ya 1-1 ugenini dhidi ya Galatasaray. Braga wana pointi tatu na klabu hiyo ya Uturuki ina moja.

Katika mechi iliyojaa ushindani mjini Istanbul, Cluj walicheza pungufu baada ya Matias Aguirregaray kutolewa kwa kadi nyekundu katika dakika ya 28 na Felipe Melo akakosa penalti kwa Galatsaray dakika saba baadaye.

Dany Nounkeu akajifunga mwenyewe na kuwapa Cluj uongozi baada ya dakika 19 kabla ya Burak Yilmaz kuwasawazishia wenyeji dakika 13 kabla ya mechi kumalizika.

Barcelona walihitaji goli la dakika za majeruhi kutoka kwa Jordi Alba na kushinda 2-1 baada ya Celtic kupata goli la kuongoza kwenye Uwanja wa Nou Camp kupitia kwa Javier Mascherano aliyejifunga kwa kichwa katika dakika ya 18 kabla ya Andres Iniesta kufunga goli kali muda mfupi kabla ya mapumziko.

Barca wanaongoza Kundi G wakiwa na pointi tisa kutokana na kushinda mechi tatu, juu ya Celtic wenye pointi nne wakati Spartak Moscow wamefikisha pointi tatu baada ya kupata ushindi wao wa kwanza, 2-1 nyumbani dhidi ya Benfica shukrani kwa goli la kujifunga la Jardel.

Valencia walihitimisha mwanzo mzuri wa asilimia 100 wa BATE Borisov katika Kundi F kupitia 'hat-trick' ya Roberto Soldado katika ushindi wa 3-0 nchini Belarus. Baada ya Bayern kushinda 1-0 ugenini dhidi ya Lille kupitia kwa penalti ya Thomas Mueller, Valencia, BATE na Bayern zote zina pointi sita huku Lille pekee ikiwa haina pointi.

No comments:

Post a Comment