Wednesday, October 10, 2012

'PICHICHI' NGUMU ZAIDI KUIPATA ULAYA NI ILE INAYOGOMBEWA NA MESSI, RONALDO NA FALCAO

Lionel Messi mshindi wa tuzo ya Pichichi msimu uliopita baada ya kufunga magoli 50. Hamna kabla yake aliyewahi kufikisha magoli 50 katika Ligi Kuu ya Hispania jambo linalomfanya Messi kuwa Pichichi (mfungaji) hatari kuliko wote waliopata kutokea katika historia.
Cristiano Ronaldo (real Madrid)
Radamel Falcao (Atletico Madrid)


MADRID, Hispania
VITA ya kuwania tuzo ya 'Pichichi' ya mfungaji bora wa Ligi kuu ya Hispania baina ya Radamel Falcao, Cristiano Ronado na Lionel Messi inatarajiwa kuweka rekodi mpya.

Baada ya mechi saba tu za kwanza za msimu, jumla ya magoli 25 tayari yameshafungwa baina ya watatu hao.

Hakuna mwingine anayekaribia rekodi hizi zinazokaribia goli moja kwa mechi katika ligi kubwa za Ulaya, isipokuwa Zlatan Ibrahimovic, ambaye amefunga magoli 9 katika mechi 8 za PSG (mechi moja zaidi ya Ligi ya Hispania). Msweden huyo hana mpinzani katika ligi kuu ya Ufaransa.

Katika Ligi Kuu ya England, mwenye magoli mengi baada ya mechi saba ni Demba Ba (Newcastle) mwenye magoli sita – moja zaidi ya Van Persie (Manchester United), Luis Suarez (Liverpool), Steven Fletcher (Sunderland) na Mhispania Michu (Swansea). Katika Ligi Kuu ya Italia (Serie A), mshambuliaji wa Uruguay, Edinson Cavani (Napoli) ndiye kinara akiwa na magoli sita, moja zaidi ya Alberto Gilardino na Miroslav Klose, wakati Mcroatia, Mario Mandzukic (Bayern Munich) anaongoza wafungaji kwenye ligi ya Bundesliga, pia akiwa na magoli sita – mawili zaidi ya wanaomkaribia.

Mabao tisa ya Falcao, karibu nusu (manne) yametokana na penalti. Cristiano Ronaldo amefunga penalti tatu na Messi penalti moja tu. Muargentina huyo ndiye pekee ambaye hajafunga kwa mguu wa kulia, lakini ndiye pekee ambaye amefunga kwa 'fri-kiki' ya moja kwa moja.

Falcao amecheza mechi chache zaidi (mechi sita) na ametumbukiza wavuni asilimia kubwa ya nafasi alizopata (33%), akimzidi Messi (21%) na Cristiano Ronaldo (18%). Mreno Ronaldo na Muargentina Messi wamefunga katika mechi nne kati ya saba walizocheza za ligi – moja pungufu ya 'The Tiger' ama 'El Tigre' Falcao, ambaye anatarajiwa kuwapa upinzani mkubwa nyota hao wawili wanaopewa nafasi kubwa ya kutwaa tuzo ya 'Pichichi'.

No comments:

Post a Comment