Wednesday, October 10, 2012

DIEGO CASTRO, MFALME WA KUPIGA PENALTI LA LIGA

Diego Castro akishangilia moja ya mabao yake

MADRID, Hispania
DIEGO Castro daima hujitokeza mbele pale linapokuja suala la kupiga penalti.

Tangu alipopanda daraja akiwa na klabu ya Sporting Gijon misimu mitano iliyopita, amefunga penalti zote alizopiga, akiwa amepiga penalti 11.

Nyingi kati ya penalti hizi zilikuwa katika wakati muhimu wa kuamua mechi. Penalti mbili alizoifungia klabu yake anayoichezea sasa ya Getafe zimeipa klabu hiyo ya mjini Madrid pointi sita, kama nyingine mbili alizofunga akiwa katika klabu yake ya zamani ya Sporting.

Hata hivyo, uwezo wake katika kufunga penalti umemwekea doa kiungo huyo wa Getafe. Ameifunga kwa penalti klabu yake ya utotoni ya Sporting.

Mafafikio ya Diego Castro katika kupiga "matuta" hayajaja haraka, kwani amejifunza taratibu kwa umakini mkubwa mbinu za kufunga penalti.

Ametengeneza staili yake kwa kuiga staili za upigaji za nyota kadhaa aliokuwa wakiwapenda tangu utotoni, akiwamo Pablo Aimar – ambaye alikuwa akimfuatilia tangu akiichezea River Plate – na pia staili ya David Villa.

Castro amekuwa katika kiwango cha juu hivi sasa, magoli yake yakiisaidia Getafe kushinda mechi mbili katika siku tano. Baada ya kuwa na wiki nzuri, mapumziko ya ligi kupisha mechi za kimataifa yamempa kocha wao wa Getafe, Luis Garcia, fursa ya kuwapumzisha wachezaji wake kabla kurejea mazoezini Jumanne.

No comments:

Post a Comment