Saturday, October 27, 2012

OKWI, SUNZU WAIPAISHA SIMBA IKIUA AZAM, TWITE APIGA TENA KAMOJA TU YANGA IKIWAZAMISHA OLJORO KWAO

Mrisho Ngassa (kushoto) wa Simba akiwaendesha wachezaji wa Azam wakati wa mechi yao ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam leo. Picha: Bongostaz.blogspot.com

EMMANUEL Okwi alifunga mara mbili na Felix Sunzu akaongeza jingine moja wakati mabingwa Simba walipowalaza Azam 3-1 na kuwapa kipigo cha kwanza msimu huu, huku Yanga nayo ikipanda hadi nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu ya Bara kufuatia ushindi wa 1-0 dhidi ya JKT Oljoro ugenini Arusha.

Ushindi huo katika mechi ya 10 umeifanya Simba ifikishe pointi 22, mbili juu ya mahasimu wao Yanga ambao walianza msimu vibaya hadi kumfukuza kocha wao aliyedumu kwa siku 80 tu, Mbelgiji Tom Saintfiet, aliyewapa ubingwa wa Afrika Mashariki (Kombe la Kagame).

Goli la pekee kutoka kwa beki Mbuyu Twite aliyesajiliwa Yanga baada ya mvutano mkali dhidi ya Simba ambao walidai kumsainisha mkataba kabla ya kutua mahasimu wao, liliipa timu hiyo inayofundishwa na Mholanzi Ernie Brandts ushindi wa sita wa msimu huu sawa na vinara, Simba.  Twite alifunga goli hilo kwa kichwa katika dakika ya 52 akiunganisha kona iliyochongwa na Haruna Niyonzima katika mechi ambayo Yanga walishambulia zaidi na kukaribia kufunga mara kadhaa ikiwamo shuti la 'fri-kiki' la Oscar Joshua kutokea nje kidogo ya boksi ambalo lilienda kugonga besela kabla ya kuokolewa na mabeki wa Oljoro katika dakika ya 30.


Kipigo kinamaanisha kwamba Azam yenye pointi 18 imeangukia katika nafasi ya tatu na hata ikishinda mechi yake ya mkononi, haitaweza kuing'oa Simba kileleni. Inaweza kurejea katika nafasi yake ya pili.

Kabla ya mechi mbili Azam zilizopita, Azam ilikuwa na nafasi ya kuing'oa Simba kileleni lakini ilishikiliwa katika sare ya 1-1 dhidi ya Ruvu Shootings ya mkoani Pwani kwenye Uwanja wa Chamazi Jumatano kabla ya kukumbana na kipigo cha leo.

John Bocco, ambaye AMEZOEA kumfunga kipa Juma Kaseja, ikiwamo 'hat-trick' aliyomfunga katika mechi ya robo fainali ya Kombe la Kagame, aliwastua mashabiki wa Simba kwa goli la mapema katika dakika ya 4 akimzidi mbio beki Mkenya Pascal Ochieng kabla ya kumchambua 'mbaya' wake Kaseja.


Hata hivyo, Simba hawakuchanganyikiwa kwa goli hilo. Walihitaji dakika mbili tu baadaye kufanya 'ubao' wa matokeo usomeke 1-1 kupitia kwa Mzambia Felix Sunzu aliyefunga kufuatia krosi safi ya winga wa Azam anayeichezea klabu hiyo ya Msimbazi kwa mkopo wa mwaka mmoja, Mrisho Ngassa.

Azam ilipata pigo baada ya mshambuliaji wao Bocco maarufu kama 'Adebayor' kuumia mapema katika dakika ya 21 na nafasi yake kuchukuliwa na Khamis Mcha. Bocco alikuwa ndio kwanza amerejea kutokea kuwa majeruhi baada ya kuikosa mechi ya Azam iliyopita dhidi ya Ruvu Shootings.  


Mganda Okwi ambaye alikuwa miongoni mwa waliotuhumiwa kucheza chini ya kiwango katika sare mfululizo zilizopita, aliipatia Simba goli la pili katika dakika ya 40 akifunga kwa kichwa mpira wa krosi ya Mwinyi Kazimoto na kuifanya timu yake iende mapumziko ikiongoza 2-1.

Okwi tena akaihakikishia Simba ushindi mnono wa kisasi cha Kombe la Kagame, ambapo Wekundu walilala 3-1, kwa kufunga bao la tatu

Furaha pekee ya Azam jana ilikuwa ni ushindi wa timu yao ya vijana wa goli 1-0 dhidi ya Simba kwenye mechi iliyochezwa mapema kwenye Uwanja wa Taifa. Bao pekee la Azam B lilifungwa na Kelvin Friday aliyepiga shuti la umbali wa mita 19 na kuwalipia kisasi kaka zao ambao walitolewa na Simba B katika nusu fainali ya michuano ya kufungua msimu ya BancABC. Simba B walitwaa taji hilo lililofanyika kwa mara ya kwanza mwaka huu na litafanyika mara nyingi mbili kwa mujibu wa mkataba wa benki hiyo ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Baada ya mechi hiyo, nahodha wa Simba, Juma Kaseja alisea waliingia uwanjani wakiwa na hofu na mechi hiyo kubwa hasa kutokana na kuwakosa nyota wao wawili muhimu kikosini kiungo Haruna Moshi 'Boban' na beki wa kati Juma Nyosso walioondolewa katika kikosi cha kwanza kutokana na makosa mbalimbali.

"Tuliingia uwanjani tukiwa na hofu kidogo kutokana na kukosekana kwa ndugu zetu hao (Boban na Nyosso)... tunashukuru Mungu tumeshinda, bado ni Wanasimba na tunaheshimu mchango wao," alisema Kaseja.

Kocha wa Simba, Mserbia Milovan Cirkovic alisema amefurahishwa na kubadilika kwa timu yake katika siku ya leo na kucheza kandanda safi tofauti na mechi zao mbili zilizopita.

Alisema mazoezi waliyofanya baada ya kurejea kutoka Tanga walikoshikiliwa kwa sare ya 0-0 dhidi ya Mgambo JKT, yamebadilisha kikosi chake na kukifanya kuwa imara zaidi.


Kocha wa Azam, Boris Bunjak alisema kuumia kwa Bocco kuliigharimu timu yake ambayo ililazimika kubadili mfumo na kucheza pasi fupi fupi badala ya mashambulizi ya kustukiza na mipira mirefu anayoitumia mshambuliaji huyo mrefu mwenye nguvu.


       
Vikosi kwenye Uwanja wa Taifa vilikuwa:

Simba:

Juma Kaseja, Nasoro Masoud 'Chollo', Amir Maftah, Pascal Ochieng, Shomari Kapombe, Jonas Mkude, Amri Kiemba/ Ramadhani Chombo 'Redondo' (dk.80), Mwinyi Kazimoto, Felix Sunzu, Mrisho Ngassa/ Edward Christopher (dk.87) na Emmanuel Okwi

Azam:
Mwadini Ali, Ibrahim Shikanda, Sahm Nuhu, Said Morad, Aggrey Morris, Abdulhalim Humud, Jabir Aziz Stima/ Kipre Balou (dk, Himid Mao/ Abdi Kassim (dk.62), John Bocco 'Adebayor'/ Khamis Mcha (dk.21), Kipre Tchetche, Salum Abubakar.

Vikosi kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid vilikuwa:

JKT Oljoro:

Luchek Mussa, Omar David, Napho Zuberi, Salim Mbonde, Marcus Raphael, Emmanuel Memba, Karagge Gunda, Meshack Nyambele, Paul Nonga, Hassan Isihaka, Swalehe Iddy.

Yanga:
Ali Mustapha 'Barthez', Shadrack Nsajigwa, Oscar Joshua, Nadir Haroub 'Cannavaro', Mbuyu Twite, Athumani Idd 'Chuji', Simon Msuva, Frank Domayo/ Nurdin Bakari (dk. 87), Didier Kavumbagu/ Jerry Tegete (dk. 78), Hamis Kiiza 'Diego' na Haruna Niyonzima.


 Msimamo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya mechi za leo:
 

                                   P      W     D     L     GF     GA      GD       Pts
1. Simba                    10      6      4     0     19        7        12        22
2.Yanga                     10      6      2     2     18      10          8        20
3. Azam                      9       5      3     1     10        6          4        18
4. Coastal Union         9       4      3     2     11        8          3        16
5. JKT Oljoro              9       2      5     3       7        9         -2         11
6. JKT Mgambo          8       3      2     3       6        4          2         10
7. Kagera Sugar         8       2      4      2       8        7          1         10
8. Prisons                   8       2      4     2       5        5           0         10
9. Ruvu Shootings      9       3      1      5      12     14          -2        10
10. Mtibwa Sugar        8       2      3     3       9        9           0          9
11. JKT Ruvu              8       2      2      4       7      13         -6          8
12. African Lyon          9       2      1      6       5      12         -7          7
13. Toto African          8       1      3      4       7       11         -4         6
14. Polisi Moro            7       0      2     5       0         8         -8         2

No comments:

Post a Comment