Tuesday, October 30, 2012

MSANII JCB ASHIKILIWA NA POLISI KWA MAUAJI ARUSHA... NI YULE ALIYETAMBA NA WIMBO "UKISIKIA PAAH, UJUE IMEKUKOSA"


Nyota wa kibao cha "Ukisikia Paah, Ujue Imekukosa" Jacob Makala a.k.a JCB a.k.a Jesus Come Back, akiwa na mpenziwe wa kizungu Diana, aliyezaa naye mtoto wa kiume hivi karibuni waliyempa jina la Makala au Albert Jacob Makala. Picha: Bongo5.com

Na Woinde Shizza, Arusha
MSANII wa muziki wa kizazi kipya kutoka jijini Arusha, Jacob Makala a.k.a JCB a.k.a Jesus Come Back aliyetamba na wimbo wa "Ukisikia Paah (Ujue Imekukosa)", pamoja na wenzake watatu wanashikiliwa na jeshi la polisi mkoani Arusha kwa tuhuma za mauaji.


Akizungumzia tukio hilo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Lebaratus Sabas alisema kuwa msanii huyo pamoja na wenzake wanashikiliwa na jeshi la polisi kwa tuhuma za kumpiga mwenzao hadi kufa katika ukumbi wa Viavia, sehemu ambayo walikuwa wanafanya shoo katika onyesho la Jambo Festival.


Alisema kuwa marehemu huyo ambaye alitambulika kwa jina la Alex Julius Samwel (21) mkazi wa Ilboru, alihudhuria onyesho la Jambo Festival lililokuwa likifanyika usiku wa Oktoba 25.


Kamanda Sabas alisema marehemu akiwa ukumbini na wenzake, alipigiwa simu na watu wanaodaiwa kuwa ni pamoja na JCB na wenzake wakimtaka atoke nje. Alitoka nje na aliporudi alionekana akitoka damu puani pamoja na kuwa na uvimbe sehemu za mwili.


"Watu wa karibu waliokuwa na marehemu walipomuuliza kwanini amevimba na anatoka damu ndipo alipowajibu kuwa alitoka nje na kufanyiwa fujo na msaniii huyo na wenzake huku akibainisha kuwa  mbali na kufanyiwa fujo pia walimchukulia simu yake ya kiganjani lakini alisema kuwa hajapata maumivu makubwa, ila kadri muda ulivyozidi kwenda ndivyo alivyozidi kuzidiwa na ndugu zake walimpeleka hospitali ya Father Babu na kufariki akiwa hospitalini hapo," alisema Kamanda Sabas.


Aliwataja watu wengine wanaoshikiliwa pamoja na JCB kuwa ni Robert Joseph (18) mkazi wa Sekei, Sara Ephraim (32) mkazi wa Engoshelaton pamoja na Remi Peter (22) mkazi wa Unga LTD.


Alisema kuwa mwili wa marehemu umehifadhiwa katika hospitali ya mkoa ya Mount Meru na watuhumiwa wote wanashikiliwa na jeshi la polisi na pindi upelelezi utakapokamilika watafikishwa mahakamani.


Katika wimbo wa "Ukisikia Paah", JCB aliwashirikisha nyota kama  Fid Q, Jay Mo na Chidi Beenz.
Kiitikio cha wimbo "Ukisikia Paah" kinasema: "Ukisikia paah ujue imekukosa, aliyelenga hana shabaha amefanya makosa."


Tuhuma dhidi ya JCB zimekuja siku chache tangu msanii mwingine wa kizazi kipya wa Arusha, Lord Eyez, kushikiliwa na polisi kwa tuhuma za kuiba vifaa vya gari la msanii mwingine Ommy Dimpoz na kujumuishwa na tuhuma za matukio mengine 30 ya wizi wa aina hiyo.


Msanii mwingine wa Arusha, Nelson Chrizostom Buchard a.k.a Father Nelly wa kundi la Xplastaz aliuawa kwa kuchomwa kisu mjini Arusha Machi 29, 2006 wakati msanii mwingine wa kizazi kipya Steve2K aliuawa 2004 kwa kudaiwa kuchomwa kisu na mtayarishaji wa muziki wake Castro Ponera. 
 

CHANZO: Gazeti la NIPASHE

No comments:

Post a Comment