Monday, October 15, 2012

MINTANGA HATIMAYE AACHIWA HURU


Shabani Mintanga (katikati) akiwa mahakamani

MAHAKAMA Kuu Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, jana ilimuachia huru aliyekuwa rais wa zamani wa Shirikisho la Ngumi Tanzania (BFT) Alhaji Shabani Mintanga baada upande wa Jamhuri kushindwa kuthibitisha ushahidi dhidi ya tuhuma za kula njama na kusafirisha dawa za kulevya kilo 4.8 aina ya heroin ya Sh. milioni 120.

Uamuzi huo ulitolewa na Jaji Dk. Fauz Twaib baada ya upande wa Jamhuri kuita mashahidi wanne dhidi ya Alhaji Mintanga lakini hata hivyo ushahidi wao umeshindwa kuishawishi mahakama kumuona mshtakiwa kuwa ana kesi ya kujibu.

Jaji Dk. Twaib alisema kuna sababu sita zilizoifanya mahakama bila kuacha shaka imuone mshtakiwa hana kesi ya kujibu.

Alisema sababu ya kwanza; upande wa Jamhuri umeshindwa kupeleka mahakamani kielelezo cha dawa au picha anazodaiwa kusafirisha Alhaji Mintanga kutoka nchini kwenda Mauritius.

Sababu ya pili; katika ushahidi wa Jamhuri na hati ya mashtaka iliyopo mahakamani, hakuna uwiano wa uzito wa dawa za kulevya ambapo hati hiyo inaonyesha ni kilo 4.8 wakati kule nchini Mauritius inaonyesha kilo 6.

Katika sababu ya tatu, jaji alisema ushahidi wa upande wa Jamhuri uliotolewa mahakamani hapo kwa nyakati tofauti ulikuwa unajichanganya kwa sababu shahaidi wa nne Charles Ulaya aliyekuwa mpelelezi wa kesi hiyo, aliiambia mahakama kuwa aliyekuwa anatafutwa ni Mika na sio Alhaji Mintanga.

“Shahidi Ulaya katika ushahidi wake alisema hamjui Alhaji Mintanga na kwamba katika upelelezi wake aliyekuwa anatafutwa kwenye kesi hiyo ni Mika,” alisema Jaji Dk. Twaib wakati akisoma sababu ya nne.
Sababu ya tano, alisema Jamhuri ingeweza kumshtaki Alhaji Mintanga kwa kosa la kula njama hata hivyo imeshindwa kuthibisha kama walikaa mahali gani kula hizo njama.

Katika sababu ya sita, Jaji Dk. Twaib alisema Kamishna wa Dawa za kulevya Kamanda Christopher Shekiondo hakwenda mahakamani kutoa ushahidi na kwamba hata taarifa za uzito wa dawa zilizodaiwa kusafirishwa kwenda Mauritiaus alizipata kwa njia ya simu.

Vielelezo pekee vilivyowasilishwa na upande wa Jamhuri ni simu ya mshtakiwa pamoja na tiketi zilizoonyesha kwamba mshtakiwa alisafiri kwenda nchini Mauritius ambavyo haviwezi kuishawishi kwamba alihusika na biashara hiyo ya dawa za kulevya.

“Kutokana na sababu hizo mahakama bila kuacha shaka imeona kwa hoja zilitolewa, mshtakiwa hakuhusika na suala hilo bali ni Mika na upande wa Jamhuri umeshindwa kuthibitisha mashtaka dhidi yake hivyo hana kesi ya kujibu na yuko huru,” alisema Jaji Dk. Twaib.

Katika kesi ya msingi, Mintanga alikuwa anadaiwa kuwa Juni 3, mwaka 2008 eneo lisilofahamika akiwa na wengine sita ambao hawajakamatwa, walikula njama ya kutenda kosa la kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroin kutoka nchini kwenda Mauritius.

Katika shitaka la pili, Mintanga alidaiwa kuwa Juni 10, mwaka 2008 akiwa na wengine sita ambao hawajakamatwa walisafirisha dawa za kulevya kilogramu 4.8 kutoka nchini kwenda Mauritius.

Alhaji Mintanga aliyekuwa amevalia suti ya 'Kaunda' ya rangi nyeusi na makubadhi ya rangi ya kahawia, baada ya kuambiwa kuwa hana kesi ya kujibu na yuko huru alionekana kama aliyepigwa ganzi pale kizimbani alipokuwa amesimama na baada ya muda mfupi aliachia tabasamu huku wanaodaiwa kuwa wanafamilia yake walionekana wakilipuka kwa furaha.

Watu wake wakiwamo watoto wake, walimkumbatia Mintanga kabla ya kuondoka naye katika viunga vya mahakama hiyo.

Mawakili wa utetezi, Jerome Msemwa na Yassin Membea, walisema baada ya kesi hiyo kuwa mahakama imeona kwamba Mintanga hakuhusika na tuhuma zilizokuwa zinamkabili na kwamba imetoa haki kwa pande zote mbili.

Wakili Membea alisema haki imetendeka kwa mteja wake pamoja na kusota mahabusu kwa zaidi ya miaka minne lakini mwisho mahakama imeona ukweli.

Mapema mwaka 2008, Mintanga alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam akikabiliwa na kesi hiyo ambapo kutokana na mashtaka yanayomkabili kutokuwa na dhamana kisheria alikuwa mahabusu hadi jana mahakama ilipomuona hana kesi ya kujibu.

No comments:

Post a Comment