Monday, October 15, 2012

INIESTA: WACHEZAJI WALIOKAMILIKA KWA KILA KITU NI FALCAO, PUYOL, XAVI, MESSI, BUSQUETS NA RONALDO...!


Iniesta (kushoto) akiwa na Lionel Messi (katikati) na Cristiano Ronaldo wakati wa ugawaji tuzo ya Mwanasoka Bora wa Mwaka wa Ulaya 2012.
BARCELONA, Hispania
Andres Iniesta anaamini kwamba straika wa Atletico Madrid, Radamel Falcao, Cristiano Ronaldo wa Real Madrid, Lionel Messi na wachezaji wengine kadhaa wa Barcelona wanaweza kuunda kikosi kikali cha soka kinachondwa na wachezaji waliokamilika kwa kila kitu

Kiungo huyo wa kimataifa wa Hispania amempongeza Falcao kutokana na uwezo wake mkubwa wa kucheza mipira ya juu na Ronaldo kwa uwezo wake mkubwa wa kupachika mabao, huku akiwamiminia sifa tele pia wachezaji wenzake kadhaa wa Barca.

"Mchezaji aliyekamilika? Ni Falcao mwenye uwezo mkubwa wa kucheza mipira ya juu, jihadi ya (Carles) Puyol, uwezo wa mguu wa kulia wa Xavi, kipaji cha (Lionel) Messi na mguu wake wa kushoto, mbinu za (Sergio) Busquets na jicho la kuchungulia goli la Cristiano Ronaldo," Iniesta aliiambia Marca.

Kiungo-mshambuliaji huyo aliendelea kumfagilia Messi, akisema kwamba hajaona mchezaji mkali duniani kama Muargentina huyo, kabla ya kuongeza kwamba straika huyo mwenye miaka 25 bado anaendelea kuimarika.

"Nimekuwa nikicheza pamoja na Leo Messi kwa muda mrefu na kwa kweli sijaona mchezaji anayefikia kiwango chake. Kila siku, kila mechi, kila mwaka, amekuwa akiongezeka kiwango. Bado mdogo sana, akiwa na muda mrefu zaidi wa kuendelea kucheza," amesema.

"Kwa heshima hiyo, mnajiona kuwa na bahati ya pekee kucheza naye katika timu moja, mkijaribu kutwaa mataji pamoja."

Iniesta hivi sasa yuko katika kikosi cha timu yake ya taifa ya Hispania kitakachoshuka dimbani kesho kucheza mechi yao ya Kundi I la kuwania kufuzu kwa fainali zijazo za Kombe la Dunia dhidi ya Ufaransa. Mechi hiyo itaanza saa 5:00 usiku kwa saa za Kibongo.

No comments:

Post a Comment