Saturday, October 13, 2012

MESSI AKARIBIA KUVUNJA REKODI YA PELE... BAADA YA KUIFUNGIA ARGENTINA MAWILI KATIKA USHINDI WA 3-0 JANA, AMEBAKIZA MAGOLI 8 AMFIKIE

'Jini' a.k.a Genius Lionel Messi

Pele

BAADA ya Lionel Messi kufunga magoli mawili katika ushindi wao wa 3-0 dhidi ya Uruguay usiku wa kuamkia leo katika kampeni za kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia 2014, mashabiki wa soka wameanza kuhesabu magoli kutoka kwa straika huyo wa Barcelona katika jaribio lake la kuvunja moja ya rekodi chache ambazo bado hajazivunja.

Muargentina huyo anakaribia kuivunja rekodi ya Mwanasoka Bora wa Dunia wa wakati wote: Pele.

Ili kutimiza hilo, Messi amebakiza kufunga magoli 8 kabla ya mwaka 2012 haujamalizika.

Edson Arantes do Nascimento, aliyefahamika zaidi kama Pele, hivi sasa ndiye anayeshikilia rekodi ya kufunga magoli mengi zaidi katika mwaka mmoja wa kalenda -- yaani kuanzia Januari hadi Desemba.

Anashikilia rekodi ya kukumbukwa pale alipofunga magoli 75 mwaka 1959, ambapo magoli 66 aliyafunga kwa klabu yake ya Santos na tisa kwa timu yake ya taifa ya Brazil.

Messi amekuwa akisambaratisha rekodi zote zilizo mbele yake na kwa mwaka huu wa Kalenda tayari amefunga jumla ya mabao 67, ambapo magoli 56 ameifungia Barcelona na 11 ameifungia timu yake ya taifa ya Argentina. Kwa ufupi, Messi alivunja rekodi yake mwenyewe mwezi mmoja tu uliopita pale alipofunga mara mbili dhidi ya Getafe, na kuipiku rekodi yake mwenyewe ya kufunga magoli 60 katika mwaka mmoja wa kalenda.

Messi ana mwezi mzima na nusu na mechi kibao za kusaka magoli hayo 8 ya kuifikia rekodi ya gwiji wa wakati wote Pele. Baada ya kuiongoza timu yake ya taifa ya Argentina usiku kuamkia leo kushinda 3-0 dhidi ya timu ngumu ya Uruguay, ambapo Sergio Aguero aliongeza la tatu, Messi ana nafasi nyingine Jumatano dhidi ya Chile, zote zikiwa ni za kuwania kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia 2014.

Pele watch-out, 'jini' anakuja huyo...

No comments:

Post a Comment