Monday, October 22, 2012

MESSI AFUNGA HAT-TRICK MARA 19, MABAO MANNE-MANNE MARA 3, MABAO MATANO MARA 1

Lionel Messi akishangili moja ya magoli yake

LIONEL Messi, ambaye alikuwa shujaa wa mechi ya ugenini ya Barcelona dhidi ya Deportivo kwenye Uwanja wa Riazor, amefunga magoli matatu au zaidi mara 23 katika maisha yake ya soka, huku 21 kati ya hizo akiwa na Barcelona na mara mbili akiwa na timu yake ya taifa ya Argentina.

Katika mechi hizo 23, amefunga 'hat-trick' mara 19. Katika mechi tatu kati ya nne zilizobaki alipiku rekodi zake mwenyewe kwa kufunga magoli manne dhidi ya Arsenal, Valencia na Espanyol na katika mechi nyingine moja 'akajifunika' kabisa mwenyewe kwa kufunga magoli matano dhidi ya Bayer Leverkusen mwaka huu katika mechi ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya.

Akizungumzia ushindi wa timu yake wa 5-4 dhidi ya Deportivo ambapo yeye alifunga 'hat trick', Messi alisema: "Tumeshinda. Daima inakuwa ngumu sana kucheza mechi tukitokea kuziwakilisha timu zetu za taifa, kwasababu unarejea ukiwa umechoka. Huu ulikuwa ni ushindi muhimu," alisema.

'Supastaa' huyo wa Argentina alisema kutokea uwanjani hakuona kama Deportivo walistahili penalti wala kutolewa kwa kadi nyekundu kwa Mascherano. "Sikuona jambo lile. niliambiwa kwamba haikutahili kuwa penalti wala kadi nyekundu, lakini hivyo ndivyo ilivyotokea na refa akaona kinyume," alisema.

Aidha, Messi alipuuza 'hat-trick' aliyofunga pamoja na magoli 59 aliyofunga katika mwaka 2012, ambayo ni rekodi kwa mchezaji wa Barcelona. Katika mwaka huu wa kalenda kuanzia Januari 2012 hadi sasa, Messi ameifungia klabu yake magoli 59 na ameifungia timu yake ya taifa ya Argentina magoli 12 na kufanya jumla ya mabao 71, manne tu pungufu ya rekodi ya wakati wote inayoshikiliwa na Pele aliyefunga magoli 75 mwaka 1959. Messi anatarajiwa kuivunja rekodi hiyo na kuweka yake ya hatari zaidi kwani bado ana zaidi ya miezi miwili ili mwaka huu 2012 umalizike Desemba 31.

"Tunachopaswa kufanya ni kuendelea kushinda, kucheza katika kiwango tulichokuwa nacho kabla ya mapumziko ya kwenda kuzitumikia timu zetu za taifa. Takwimu za 'hat-trick' si muhimu, kushinda mechi zetu ndiyo muhimu, pamoja na kuchangia mafanikio ya klabu," alisema.

No comments:

Post a Comment