Saturday, October 27, 2012

CELTIC: THAMANI YA MKENYA VICTOR WANYAMA NI BIL.63/-

Victor Wanyama

Tulia weweeee...! Mkenya Wanyama (kushoto) akichuana na Andres Iniesta wa Barcelona wakati wa mechi yao ya Kundi G la Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya kwenye Uwanja wa Camp Nou Jumanne Oktoba 23, 2012.
SCOTLAND
KOCHA Neil Lennon wa Celtic ametaja thamani ya Victor Wanyama kuwa ni paundi za England milioni 25 (Sh. bilioni 63) baada ya kuthibika kuwa kiungo huyo wa kimataifa wa Kenya amekataa ofa aliyopewa ya kusaini mkataba mpya.

Lakini kocha huyo amesisitiza kwamba Celtic haiko katika "shinikizo la kumuuza" la kumuuza kiungo huyo mwenye miaka  21 na ambaye amemuweka katika daraja la juu kiasi cha kuweza kuichezea Barcelona.

"Ni paundi milioni 25," amesema Lennon wakati alipotakiwa kutaja thamani ya mchezaji huyo.


"Hivi sasa dunia iko chini ya miguu ya Wanyama.

"Lakini miguu yake iko hapa na haiendi kokote labda sisi tutake hivyo."

Kiungo huyo alijiunga Julai 2011 kwa ada 'kiduchu' ya paundi za England 900,000 (Sh. bilioni 2.3) akitokea katika klabu ya Ligi Kuu ya Bulgaria ya Beerschot, akisaini mkataba wa miaka minne.

Wanyama amesema amekataa ofa kutoka katika klabu ya Ligi Kuu ya England ya Aston Villa iliyotaka kumng'oa Celtic Park na kiwango chake cha juu katika klabu yake inayoshikilia ubingwa wa Ligi Kuu ya Scotland kimemfanya ahusishwe na uhamnisho wa kujiunga na klabu nyingine kadhaa za Ligi Kuu ya England.


Alipoulizwa kama bei hiyo ya paundi milioni 25 inaendana na yosso huyo, Lennon alijibu: "Sijui, lakini hiyo ndiyo thamani ninayoiweka kwake.

"Nadhani ana kipaji cha hali ya juu na pia anaweza kuimarika zaidi."

Wanyama alisifiwa kutokana na kiwango cha juu alichoonyesha dhidi ya Barcelona, wakati Celtic walipokuwa wamebakiza sekunde 15 tu kupata sare ya ugenini ya 1-1 dhidi ya vigogo hao wa Hispania katika mechi yao ya Kundi G la Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya kwenye Uwanja wa Nou Camp. 


Hata hivyo, kina Wanyama walipigwa 2-1 kutokana na goli la Jordi Alba katika dakika ya 93 na sekunde ya 45 ya mechi hiyo iliyokuwa imeongezwa dakika 4 za majeruhi.

Alipoulizwa kama kiungo huyo ana kiwango cha juu kiasi cha kuweza kuichezea Barcelona, Lennon alijibu: "Nadhani anaweza, ndiyo.

"Kama ofa zikija, hakutakuwa na shinikizo la kumuuza. Sisi ndiyo tutakaoamua. Hatutamuuza kwa sababu ana mkataba mrefu."

Lennon ameeleza vilevile kwamba amesikitishwa na wakala wa mchezaji huyo, Rob Moore, aliyesema hadharani kwamba Wanyama amekataa kusaini mkataba mpya kwa sababu haujafikia matarajio yake.


"Tunaweza kumuendea tena, lakini tumempa mkataba wenye mshahara ulioboreshwa zaidi," kocha huyo ameongeza.
 

"Hatupaswi kufanya hivyo, lakini tunadhani kwamba ni zawadi anayostahili kutokana na kiwango chake.

"Ni jambo zuri kwa klabu na bodi na ninakubaliana na falsafa hii ya kuboresha mishahara ya wachezaji kwa kuangalia viwango vyao."

No comments:

Post a Comment