Mshindi wa Redd's Miss Talent 2012, Babylove Kalala akionyesha umahiri wake wa kuchezea nyoka aina ya chatu uliompa ushindi wa taji la Miss Talent |
Mshiriki namba 16 kutoka Kanda ya Mashariki, Irene Verda akionyesha umahiri wake wa kupuliza saxophone. |
Babylove Kalala akionyesha ujasiri wa kumuuma wakati mrembo huyo na wenzake wanaowania taji hilo walipotembelea eneo la Snake Park mjini Arusha. |
Na Mwandishi wetu
MREMBO kutoka Kagera anayewakilisha Kanda ya Ziwa katika shindano la Redd’s Miss Tanzania, Babylove Kalala juzi usiku alitwaa taji la Redd’s Miss Talent lililofanyika kwenye hoteli ya Giraffe, iliyopo Kunduchi, Dar es Salaam.
Kutokana na ushindi huo, Babylove sasa anaungana na Miss Photogenic, Lucy Stephano na Redd's Miss Tanzania Sports Lady, Mary Chizi kuingia hatua ya 15-Bora ya fainali ya Redd’s Miss Tanzania itakayofanyika mwishoni mwa wiki.
Babylove aliwashinda warembo wengine 29 aliokuwa anachuana nao baada ya kuonesha kipaji cha hali ya juu wakati akicheza ngoma kwa kutumia nyoka, kiumbe ambaye warembo wengine walionekana kumuogopa mno.
Warembo wengine walioingia hatua ya 5-Bora ya Miss Talent walikuwa ni Joyce Baluhi na Irene Verda wa Kanda ya Mashariki, Catherine Masumbigana (Temeke) na Brigit Alfred (Kinondoni).
Mgeni rasmi katika shindano hilo alikuwa Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Catherine Magige ambaye aliwataka warembo wanaoshiriki kutumia mashindano hayo kama chachu ya kufikia malengo waliyojiwekea.
Akizungumza mara baada ya kutwaa taji hilo, Babylove aliwashukuru washiriki wengine kwa kuwa chachu ya yeye kuhakikisha anakuwa mbunifu zaidi, huku akiahidi kufanya makubwa katika shindano la Redd’s Miss Tanzania.
Shindano la Redd’s Miss Tanzania kwa sasa linadhaminiwa na kinywaji cha Redd’s Original kinachozalishwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL).
No comments:
Post a Comment