Friday, October 5, 2012

GERVINHO: "KAZIBURE" WA MWAKA JANA ANAYECHOMOKA KUTOKA KATIKA KIVULI CHA RVP








WATABIRI walibashiri matatizo makubwa sana kwa Arsenal pale Robin van Persie alipofungasha mizigo yake na kuelekea Old Trafford katika kipindi kilichopita cha usajili lakini pengine hawakupaswa kuingiwa na hofu.

Gervinho, ambaye alicheza msimu wake wa kwanza London kaskazini katika kivuli kikubwa cha "Dutch Master" RVP, hatimaye amerejea katika kiwango chake kilichomshawishi kocha Arsene Wenger kumsajili kutoka Lille huku Mjerumani Lukas Podolski, akithibitisha yeye ni mmoja wa wafungaji "natural" wa Ulaya.

Wakati Van Persie akifunga magoli 37 msimu uliopita, utani wa kuitwa "timu ya mtu mmoja" ulielekezwa mara kwa mara kwa Arsenal lakini kuondoka kwake, kumemfungulia Gervinho, ambaye hakuwa akipendwa na mashabiki wa Gunners, njia ya kuja kuwa mmoja wa mastraika wakali.

Gervinho alifunga magoli manne tu ya Ligi Kuu ya England msimu uliopita na hakufunga hata moja katika Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya na mchezaji huyo wa Ivory Coast akapachikwa jina la "Kazi Bure" na mashabiki wa soka wa Tanzania kutokana na kufanya kazi kubwa ya kupunguza mabeki lakini isiyo na matunda kutokana na kuishia kulenga nje ya lango huku mashuti yake mengi yakiishia "kuzitesa" nyavu za pembeni ya lango.

Kiwango kibovu kilimhakikishia nafasi ya kudumu ya kukaa benchi hasa aliporejea kutoka kwenye fainali za Mataifa ya Afrika mapema mwaka huu.

Alionekana kuwa mchezaji ambaye "hafiti" kwenye kikosi na mashabiki wachache sana wa klabu hiyo waliowahi japo kufikiria kwamba angeweza kukaribia kwa namna yoyote kuziba pengo la Van Persie.

Baada ya kufunga goli la kuongoza katika ushindi wa kiwango kisichovutia cha Arsenal wa 3-1 dhidi ya Olympiakos katika Ligi ya Klabu Bingwa Jumatano na kuendeleza mwanzo wake mzuri wa msimu, kuna ishara kwamba mchezaji huyo anayesifika kwa kufanya kazi kwa bidii, aliyesajiliwa kama winga, ameanza kukubalika Emirates.

Hivi sasa amefunga magoli matano katika mechi tano zilizopita, matatu katika Ligi Kuu na mawili Ulaya.

"Anafunga magoli, hivyo kujiamini kwake kuko juu," alisema kocha msaidizi Steve Bould kuhusu Gervinho, ambaye pia alimpikia Podolksi goli muhimu la pili mapema katika kipindi cha pili dhidi yaOlympiakos.

"Nadhani ushirikiano wake uwanjani umeanza kuwa bora. Anajizoesha kucheza kama mshambuliaji wa kati. Sidhani kama ameshacheza katika nafasi ile mara nyingi lakini ni hatari kwa kasi yake na chenga wakati mwingine. Anaweza kuja kuwa mchezaji mkali sana."

Anahitaji kufanya juhudi zaidi ili kuja kufikia matawi wa mawinga waliobadilishwa na Wenger na kuwa washambuliaji hatari wa kati kama, Thierry Henry, lakini kiwango chake na uelewano wake na Podolski na kiungo mchezesha timu Santi Cazorla unamaanisha kwamba idadi ya mabao ya Arsenal msimu huu haitamtegemea mtu mmoja.

"Kama atamkaribia tu Thierry Henry itakuwa ni bab'kubwa," Bould aliongeza. "Anajifunza na anakwenda vyema. Nimefurahishwa sana."

Mchango wa Podolski haushangazi. Licha ya kutokuwa na kasi na ufundi kama wa Van Persie, njaa ya goli anayo sawa na Mholanzi huyo iliyomfanya kuwa wafungaji waliotisha katika Bundesliga na kuwamo katika kikosi cha timu ya taifa ya Ujerumani tangu mwaka  2004.

"Podolski ni muuaji na tunatarajia hali hiyo iendelee," Bould alisema.

Arsenal wako kileleni mwa Kundi B la Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya wakiwa na pointi sita na huku wakiwa hawajacheza mechi zote mbili dhidi ya Schalke, wako katika nafasi nzuri ya kutinga hatua ya 16.

No comments:

Post a Comment