Saturday, October 6, 2012

FERGUSON: CHRISS SMALLING ANAWEZA KUCHEZA KESHO DHIDI YA NEWCASTLE

Chris Smalling
MANCHESTER, England
Kocha Alex Ferguson wa Manchester United amefichua leo kwamba beki Chris Smalling anaweza kushuka dimbani kwa mara ya kwanza msimu huu kesho wakati watakapocheza mechi yao ya Ligi Kuu ya England dhidi ya Newcastle United.

Beki huyo wa kati amekuwa nje tangu alipovunjika mguu wakati wa maandalizi ya msimu, lakini amekuwa akishiriki vyema mazoezi kwa wiki kadhaa sasa na hivyo anaweza kuvaa uzi wa Man U katika mechi yao ya ugenini kesho kwenye Uwanja wa Sports Direct Arena.

Huku Phil Jones na nahodha Nemanja Vidic wakiwa bado majeruhi, Ferguson amefurahia kurejea kwa Smalling kikosini.

"Smalling ana nafasi ya kuwamo kikosini - Jones na Vidic, ni wazi kwamba hawatakuwamo," Ferguson ameiambia Sky Sports.

"Ashley Young ataanza mazoezi wakati mechi za kimataifa zitakapoanza, hasa katika wiki ya pili.

"Hivi sasa, Young anaweza kucheza katika mechi dhidi ya Stoke lakini, ni wazi kwamba Smalling, atakuwa ameshafanya mazoezi ya kutosha ya kuchezea mpira na hivyo kuwa na nafasi ya kucheza Jumapili. Kwavile tumekuwa na matatizo katika sehemu ya ulinzi wa kati, hii ni habari njema kwetu."

No comments:

Post a Comment