Wednesday, October 10, 2012

FALCAO HUFUNGA GOLI KATIKA KILA DAKIKA 45

Radamel Falcao

MADRID, Hispania
HAKUNA anayebisha kwamba Falcao ni straika bora duniani hivi sasa. Kila anachogusa mchezaji huyo wa Atletico Madrid hugeuka dhahabu kwa sasa na kutokana na magoli yake anayofunga amepata nafasi ya kuongoza katika mbio za kuwania tuzo ya Ballon d'Or ya Mwanasoka Bora wa Dunia.

Hivi sasa, straika huyo anayefahamika pia kama 'The Tiger' amefunga goli katika kila dakika 45 alizokuwa uwanjani. Kufikia sasa msimu huu, amefunga magoli 12 katika dakika 551 alizokuwa uwanjani. Kutokana na mechi 10 ambazo timu yake ya Atletico imecheza kwenye Ligi Kuu ya Hispania 'Liga BBVA', Kombe la Super Cup la Ulaya na Ligi ya Europa, Mcolombia huyo amecheza mechi saba na amefunga magoli sita.

'Hat-trick' mbili alizofunga dhidi ya Chelsea na Athletic Bilbao, pamoja na magoli mawili-mawili aliyofunga dhidi ya Real Betis na Malaga na goli lake moja-moja dhidi ya Rayo Vallecano na Valladolid, yanathibitisha kwamba Falcao ndiye 'mdunguaji' anayeongoza duniani kwa sasa.

Ameshindwa kufunga goli katika mechi moja tu, dhidi ya Levante katika mechi yao ya kwanza ya ligi. Pia hakufanya mambo yake anayoyaweza zaidi dhidi ya Espanyol, Hapoel na Viktoria Plzen, kwa sababu hakucheza.

Baada ya kushindwa kufunga goli katika dakika 94 kwenye Uwanja wa 'Ciutat de Valencia', Falcao alirejea kwa kufunga magoli matatu dhidi ya Athletic Bilbao – ambapo alipumzishwa katika dakika ya 81 ili apumzike kidogo kabla ya mechi yao ya ugenini Monaco.

Wakati wa mechi ya fainali ya Super Cup ya Ulaya aliishangaza dunia nzima kwa kufunga 'hat-trick' nyingine kali dhidi ya mabingwa wa Ulaya, Chelsea, na wakati mechi ikiwa imeshaamuliwa, kocha Diego Simeone alimpumzisha katika dakika ya 87 ili mashabiki wampigie makofi.

Kwenye La Liga, alifunga goli dhidi ya Rayo Vallecano, ambapo alicheza kwa dakika 93. Licha ya kuwa na maumivu madogo ya misuli ya paja, aliboresha rekodi yake ya kufunga dhidi ya Valladolid –goli moja katika dakika 47– na Betis –magoli mawili katika dakika 54. Na mwishowe, baada ya wiki mbili bila ya kucheza, alirejea dhidi ya Malaga na 'akatupia' mengine mawili ndani ya dakika 95.

No comments:

Post a Comment