Wednesday, October 10, 2012

RONALDO AZIDI KUIFUKUZIA REKODI YA MAGOLI YA RAUL MADRID

Ronaldo (kulia) akishangilia na Raul, kabla ya gwiji huyo hajaondoka Real Madrid

MADRID, Hispania
KWENYE Uwanja wa Nou Camp, Cristiano Ronaldo alifunga goli lake la 160 na la 161 la mechi za kimashindano akiwa na jezi ya Real Madrid.

Raul alitumia misimu 16 kufikisha magoli 323, ambayo ndiyo rekodi ya wakati wote ya klabu hiyo, wakati Ronaldo tayari amefikisha nusu (49.8%) kwa misimu mitatu tu.

Cristiano hivi sasa anashika nafasi ya tisa katika orodha ya wafchezaji waliofunga magoli mengi zaidi katika historia ya Real Madrid, akiwa amempita Amancio Amaro – ambaye alifunga magoli 155 katika misimu 14 – katika mechi dhidi ya Deportivo.

Hata hivyo, ni wastani wa kufunga magoli mengi ndio unaomfanya Ronaldo abaki kuwa wa kipekee: katika misimu mitatu kamili kufikia sasa akiwa na klabu hiyo, amefunga wastani wa magoli 48.6 kwa msimu. Kwa maneno mengine, wakati Raul alihitaji kucheza mechi 741 ili kuweka rekodi hiyo, Ronaldo amefikia nusu yake kwa kucheza mechi 155 tu.

Kama Ronaldo ataendelea na kasi yake na kumaliza miaka mitatu iliyobaki kati ya sita ya mkataba wake wa sasa, inamaanisha kuwa atafikisha jumla ya magoli 292, ambayo yatakuwa ni magoli 31 pungufu ya rekodi ya Raul – pengo ambalo ni dogo kwa mtu ambaye alifunga magoli 54 katika msimu wa 2010-11 na magoli 60 katika msimu 2011-12 katika michuano yote.

Kati ya wachezaji nane walio mbele ya CR7 katika orodha ya wafungaji bora wa wakati wote Madrid (Butragueno na Pirri, ambao wamelingana katika magoli 171, ndio wanaotarajiwa kufuatia kupitwa na mshambuliaji huyo mzaliwa wa Madeira, Ureno), huku Ferenc Puskas (mwenye wastani wa goli 0.92 kwa mechi) ndiye pekee mwenye wastani mzuri zaidi ya Ronaldo katika kufumania nyavu.

No comments:

Post a Comment