Monday, October 8, 2012

CRISTIANO RONALDO AWEKA REKODI 'EL CLASICO' YA BARCELONA NA REAL MADRID... NI BAADA YA KUTUPIA MABAO MAWILI JANA NA HIVYO KUWA MCHEZAJI PEKEE KUFUNGA KATIKA MECHI SITA MFULULIZO ZA CLASICO..!

Tulieni... tulieni...! Cristiano Ronaldo wa Real Madrid akishangilia baada ya kufunga goli la kwanza wakati wa mechi yao ya 'el clasico' katika La Liga, Ligi Kuu ya Hispania dhidi ya Barcelona kwenye Uwanja wa Camp Nou jana usiku, Oktoba 7, 2012. (Picha: Reuters)


Cristiano Ronaldo wa Real Madrid (kulia) akimtoka Sergio Busquets wa Barcelona wakati wa mechi yao ya 'el clasico' katika La Liga, Ligi Kuu ya Hispania dhidi ya Barcelona kwenye Uwanja wa Camp Nou jana usiku, Oktoba 7, 2012. (Picha: Reuters)

Ronaldo (kulia) akishangilia goli la pili na wenzake wakati wa mechi yao ya 'el clasico' katika La Liga, Ligi Kuu ya Hispania dhidi ya Barcelona kwenye Uwanja wa Camp Nou jana usiku, Oktoba 7, 2012. Ilimalizika kwa sare ya 2-2. (Picha: Reuters)
MADRID, Hispania
Cristiano Ronaldo ametokea kuwa na 'mzuka' wa kupachika mabao kila mara anapocheza dhidi ya Barcelona na amethibitisha hilo kwa mara nyingine jana usiku pale alipofunga mabao yote mawili ya Real Madrid wakati wakitoka sare ya 2-2 dhidi ya Barca katika 'el clasico' yao ya La Liga, Ligi Kuu ya Hispania.

Kutokana na mabao aliyofunga jana  kwenye Uwanja wa Camp Nou, Ronaldo ameandika rekodi kwa kuwa mchezaji wa kwanza katika historia kuwahi kufunga katika mechi sita mfululizo za 'el clasico' ya mahasimu wa jadi, Barcelona na Real Madrid.

Ronaldo alianza kasi yake katika robo fainali ya Kombe la Mfalme msimu uliopita, akifunga katika mechi ya kwanza kwenye Uwanja wa Santiago Bernabeu na ya marudiano kwenye Uwanja wa Camp Nou.

Aliendeleza makali yake katika mechi ya marudiano ya La Liga, Ligi Kuu ya Hispania iliyochezwa April 21 wakati alipofunga goli lililowapa Real Madrid ushindi wa 2-1 na kuwasafishia njia ya kutwaa ubingwa msimu uliopita wa 2011/2012.

Wakati walipokutana katika mechi mbili za kuwania taji la Super Cup mwanzoni mwa msimu huu, Cristiano pia alifunga katika mechi zote na kuisaidia Real kutwaa taji hilo kabla ya jana kufunga tena mabao yote mawili ya Real Madrid.

No comments:

Post a Comment