Monday, September 24, 2012

WAJERUMANI KUTIKISA BAGAMOYO KWA IGIZO LA ATALANTA


KUNDI la Das Letzte Kleinod kutoka Ujerumani kesho Jumanne litafanya onyesho la mchezo wa kuigiza  wa ATALANTA unaozungumzia masuala ya utekaji nyara na uharamia wa meli katika pwani ya Somalia.

Mchezo huo ambao umelenga kualezea masuala mbalimbali ikiwamo madhara yatokanayo na uharamia huo unaofanyika katika pwani ya Somalia kwa zaidi ya miaka 20, utaonyeshwa katika Tamasha la Sanaa na Utamaduni la Bagamoyo na baadaye utaonyeshwa kwenye ukumbi wa Goethe Institute jijini Dar es Salaam Ijumaa.

Kwa mujibu wa mratibu wa kikundi hicho, Juliane Lenssen, mchezo huo  wa ATALANTA umeandaliwa kutokana na ripoti iliyotokana na utafiti uliofanywa na mwandishi na muongozaji wa mchezo huo Jens-Erwin Siemssen katika pwani ya Somalia, na pwani za Afrika Masharki.

Amesema kundi hicho kimepata mwaliko wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kuja Tanzania kuonyesha mchezo huo ambapo pia umeshirikisha wasanii wawili kutoka Tanzania, mmoja kutoka Kenya na wengine kutoka Ujerumani.

Huu ni mchezo wa pili kwa kikundi hiki kutengeneza kuhusisna na masuala mbalimbali ya Afrika ambapo mwaka 2007, kikundi hiki kiliandaa mchezo wa "Mkono wa Damu" ambao ulikuwa ukizungumzia masuala mbalimbali ya utumwa ambao ulionyeshwa katika nchi mbalimbali na kwa hapa Tanzania ulionyeshwa katika miji ya Bagamoyo na Zanzibar.

No comments:

Post a Comment