Sunday, September 23, 2012

VAN PERSIE AIZAMISHA LIVERPOOL, ARSENAL WAISHIKA MANCHESTER CITY, DEMBA BA AIPA USHINDI NEWCASTLE DHIDI YA NORWICH, DEFOE AIPA RAHA TOTTENHAM...MILAN, INTER ZACHAPWA!


LONDON, England
PENATI ya Robin van Persie kuelekea mwishoni mwa mechi iliipa Manchester United iliyocheza chini ya kiwango ushindi wa ugenini wa 2-1 dhidi ya wachezaji 10 wa Liverpool katika mechi yao iliyojaa hisia ya Ligi Kuu ya England kwenye Uwanja wa Anfield huku mabingwa watetezi, Manchester City wakishikiliwa kwa sare ya nyumbani ya 1-1 dhidi ya Arsenal leo.

Mholanzi Van Persie aliwahakikishia ushindi Man U wakati alipopiga penati ya shuti kali iliyomshinda kipa Pepe Reina kufuatia Glen Johnson kumuangusha Antonio Valencia.

Licha ya kucheza chini ya kiwango, Man U walipanda hadi katika nafasi ya pili katika msimamowa ligi wakiwa na pointi 12, wakizidiwa kwa pointi moja tu na vinara Chelsea.

Man City walipata sare ya tatu katika mechi zao tano za mwanzo wa msimu baada ya  Laurent Koscielny kuisawazishia Arsenal kwa bao la 'usiku' kufuatia goli la utangulizi la Joleon Lescott kuwapa wenyeji uongozi hadi mapumziko. Timu zote mbili hazijafungwa na kufikisha pointi tisa.

Tottenham Hotspur wamefikisha pointi nane baada ya Jermain Defoe kuwafungia bao la ushindi wa 2-1 dhidi ya Queens Park Rangers, ukiwa ni ushindi wa kwanza wa nyumbani wa Tottenham chini ya kocha Andre Villas-Boas.

Demba Ba alifunga bao pekee lililowapa Newcastle United ushindi wa 1-0 dhidi ya Norwich City inayonolewa na kocha wao wa zamani, Chris Hughton.

Hiyo ilikuwa ni mechi ya kwanza kwenye Uwanja wa Anfield tangu kutolewa kwa taarifa ya  Hillsborough iliyowasafisha mashabiki wa Liverpool ambao awali walikuwa wakilaumiwa kwa kusababisha vifo vya mashabiki 96 kwenye mechi yao ya nusu fainali ya Kombe la FA mwaka 1989.

Balaa kwa Liverpool lilianza katika dakika ya 39 wakati mchezaji wao Jonjo Shelvey alipotolewa nje kwa kadi nyekundu.

Hata hivyo, Liverpool walipata bao walilostahili baada ya kuanza kipindi cha pili kupitia shuti la Steven Gerrard, lakini Man U wakasawazisha dakika sita baadaye kupitia shuti la "upinde" la beki Rafael.

Bao la 'usiku' la Van Persie, ambalo ni la tano kwake msimu huu, limemuacha kocha Brendan Rodgers akikosa ushindi baada ya mechi tano za mwanzo wa msimu, ikiwa ni rekodi "mbovu" kabisa katika historia ya klabu hiyo kwenye Ligi Kuu ya England.

No comments:

Post a Comment