Alain Mulumba Kashama |
ONYESHO la Usiku wa Sauti na Marafiki wa kweli ambalo litakaowakutanisha wanamuziki mbalimbali waliowahi kupigia bendi ya Diamond Sound 'Dar es Salaam Kibinda Nkoi' pamoja na wanamuziki wengine nyota nchini utafanyika mwezi ujao.
Meneja Uhusiano wa Kampuni ya Endless Fame inayoandaa onyesho hilo, Zulfa Msuya amesema mjini Dar es Salaam kuwa, kusogezwa mbele kwa onyesho kumetokana na baadhi ya wanamuziki kuwa safarini huku wengine wakiwa katika kazi ya kurekodi na bendi zao.
“Tumelazimika kusogeza mbele onyesho hili kwa sababu walengwa wakuu walikuwa safarini, wengine walikuwa wana kazi ya kurekodi, kwa hiyo hawakuweza kuanza mazoezi kwa muda uliotakiwa, lakini sasa wamesharejea wote na wako tayari kuanza kambi kwa ajili ya siku hiyo,” amesema.
Zulfa amesema wanamuziki hao watakuwa wakifanya mazoezi katika ukumbi wa Princess Hall pale Sinza, Mapambano na mazoezi hayo yatachukuwa wiki mbili.
Naye kiongozi wa Diamond Sound, Ibonga Katumbi ‘Jesus’ amesema wanataka kufanya onyesho ambalo litakuwa historia, hivyo bila timu yote kukamilika isingekuwa rahisi wao kuanza mazoezi.
“Sisi hatujakaa pamoja zaidi ya miaka 12, ili kupata muziki wenye kiwango cha juu ni lazima tukae si chini ya wiki mbili kufanya mazoezi, ili watu wasikie ladha ile ile waliyokuwa wakisikia TCC, Silent Inn.
“Wasisahau kuwa tutapiga pia nyimbo za Beta Musica, sasa mtu kama Adolph hakuwepo Beta, Kata Nyama amepiga Beta wimbo mmoja, lakini kuna wanamuziki kaka zetu watakuwepo pia nyimbo zao ni za miaka ya 1980 huko nao lazima zifanyiwe mazoezi, tuko makini kuhakikisha tunafanya hili kwa ufanisi mkubwa,” amesema.
Jesus amesema kuanzia wiki ijayo utaratibu wa muda wa kuanza mazoezi, ukumbi na matangazo mengine mbalimbali yataanza kutoka kwa nguvu kwenye vyombo vya habari.
Ameongeza pia kuwa hata nyimbo zingine zitaanza kusikika katika mapigo tofauti lakini zikiimbwa na wanamuziki wote wa zamani.
No comments:
Post a Comment