Goooooohh..! Straika Falcao akishangilia goli alilotupia |
Radamel Falcao |
MADRID, Hispania
Radamel Falcao alifunga mara mbili
wakati Atletico Madrid ikicharuka kutoka kuwa nyuma na kushinda ugenini kwa
mabao 4-2 dhidi ya Real Betis, hivyo kupanda hadi nafasi ya pili katika msimamo
wa La Liga, Ligi Kuu ya Hispania jana usiku.
Straika huyo wa kimataifa wa Colombia
aliye katika kiwango cha juu aliongeza idadi ya mabao yake na kufikia saba katika
mechi tano baada ya kupiga shuti lililokwenda wavuni na kuongeza jingine la
penati mara baada ya mpira kuanzishwa tena, hivyo kujiweka kileleni mwa
wafungaji wanaoongoza kwa mabao katika La Liga huku akiwaacha nyota Lionel
Messi wa Barcelona mwenye mabao sita na Cristiano Ronaldo aliyefikisha mabao
matatu.
Watokea benchi Diego Costa na Raul
Garcia walikamilisha ushindi wa Atletico Madrid wakati Betis walipomaliza mechi
wakiwa tisa uwanjani na kuwasaidia mabingwa wa Ligi ya Europa (Atletico Madrid)
kufikisha pointi 13 kutokana na mechi tano, pointi mbili kabla ya kuwashika
vinara Barcelona.
Betis walipata goli la utangulizi
katika dakika ya 25 wakati mpira wa krosi ya Salvador Agra ulipodunda ndani ya eneo
la hatari na beki wa Atletico, Miranda akajifunga katika harakati za kuokoa.
Iliwachukua dakika mbili tu Atletico kusawazisha
bao hilo baada ya Falcao kuiwahi krosi ya chini ya Raul Garcia na kufunga.
Kipa wa Betis, Casto Espinosa aliiokoa
timu yake mara kadhaa na kabla ya mapumziko wakaongoza tena, safari hii krosi
ya Juan Carlos ikaenda moja kwa moja wavuni baada ya kumpita beki Juanfran wa
Atletico.
Atletico wakasawazisha tena kwa haraka.
Falcao akaangushwa na refa akatoa penati mara tu baada ya mpira kuanzishwa,
uamuzi uliopingwa na wachezaji wa Betis ambao mwishowe ulimfanya beki wao Damien
Perquis apewe kadi nyekundu ya kiaktili, na Mcolombia Falcao akafunga penati
hiyo.
Falcao, aliyekuwa akisumbuliwa na
maumivu ya paja kabla ya mechi hiyo, alitolewa na nafasi yake ikatwaliwa na Costa
na mshambuliaji huyo Mbrazil akaipa tena uongozi Atletico kutokana na mpira wa
kona.
Wenyeji wakajikuta kwenye wakati mgumu
zaidi wakati mtokea benchi Joel Campbell alipotolewa nje kwa kadi ya pili ya
njano katika dakika ya 83.
Raul Garcia aliifungia Atletico bao la
nne na kuiacha Betis ikiwa katika nafasi ya sita kutokana na pointi tisa baada
ya kumalizika kwa mechi hiyo iliyoahirishwa awali mwanzoni mwa mwezi huu.
No comments:
Post a Comment