Sunday, September 16, 2012

TP MAZEMBE YA SAMATTA YACHEZEA KICHAPO GHANA... SASA YAANGUKIA MDOMONI MWA MABINGWA ESPERANCE KATIKA NUSU FAINALI KLABU BINGWA AFRIKA

Waleteni sasa hao Esperance...! Straika Mbwana Samatta wa TP Mazembe.
ACCRA, Ghana
JARIBIO la klabu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kutaka kumaliza kileleni mwa msimamo wa Kundi B la Ligi ya Klabu Bingwa Afrika limegonga mwamba leo baada ya kukubali kipigo cha ugenini cha bao 1-0 kutoka kwa Berekum Chelsea ya Ghana huku mahasimu wao katika kundi hilo, Al Ahly ya Misri ikipata sare ya 1-1 dhidi ya Zamalek na kukwea kileleni. 


Ahly imeongoza Kundi B baada ya kumaliza ikiwa na pointi 11 huku Mazembe wanayoichezea mastraika wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu, ikimaliza katika nafasi ya pili baada ya kufikisha pointi 10. 


Kabla ya mechi za jana, Mazembe na Ahly zilishafuzu kwa hatua ya nusu fainali, lakini kila moja ilikuwa ikiwania kumaliza kileleni ili kuwakwepa mabingwa watetezi, Esperance ya Tunisia ambao walimaliza kileleni katika Kundi A.


Mshambuliaji Jordan Opoku wa Chelsea ndiye aliyezima ndoto za kina Samatta kumaliza wa kwanza katika kundi lao baada ya kufunga goli pekee wakati zikiwa zimesalia dakika 10 kabla ya kumalizika kwa muda wa kawaida wa mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Ohene Djan Sports jijini Accra.


Mazembe sasa wameangukia mdomoni mwa vigogo Esperance ambao watavaana nao Oktoba 10 huku vinara Ahly wakiwakabili Sunshine Stars ya Nigeria waliomaliza katika nafasi ya pili kwenye kundi lao la A.

No comments:

Post a Comment