Sunday, September 16, 2012

MAJAJI WATATU KUANZA KUPITIA UMRI UMRI WA LULU KESHO JUMATATU… MAWAKILI WATAKA ACHUKULIWE KUWA NI MTOTO KWANI ND’O KWANZA AMEFIKISHA MIAKA 17

Lulu kabla ya kukumbwa na matatizo yaliyompeleka mahabusu.

Sakata la umri wa msanii wa filamu, Elizabeth Michael maarufu kama Lulu litaanza kutafutiwa ufumbuzi kesho wakati jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufani litakapoketi ili kuanza kupitia maombi yanayohusiana na umri wa msanii huyo.

Katika kesi ya msingi, Lulu anashtakiwa kwa mauaji ya msanii mwenzake Steven Kanumba (28).

Majaji watatu watakaoketi kusikiliza maombi hayo ni Bernard Luanda, January Msoffe na Katherine Oriyo.

Hatua hiyo inafuati upande wa Jamhuri kupinga uamuzi wa Jaji Dk. Fauz Twaib wa Mahakama Kuu Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, aliyekuwa amekubali kusikiliza maombi ya kuchunguza umri wa Lulu..

Hati ya mashtaka ya kesi hiyo imeeleza kuwa Lulu ana umri wa miaka 18 wakati mawakili wa upande wa utetezi, Kennedy Fungamtama, Peter Kibatala na Fuljence Massawe wanadai kuwa cheti cha kuzaliwa cha msanii huyo kinaonyesha ana miaka 17, hivyo kesi yake ihamishiwe
kwenye mahakama ya watoto.

Awali, maombi hayo yaliwasilishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu lakini yalikataliwa na hivyo mawakili wa Lulu wakalazimika kuyawasilisha Mahakama Kuu ambayo katika uamuzi wake, ilikubali kufanya uchunguzi wa umri halali wa mshatakiwa huyo.

Lulu anadaiwa kuwa Aprili 7 mwaka huu, alimuua Kanumba katika eneo la Sinza Vatican, jijini Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment