Thursday, September 13, 2012

TFF KUTOA VIFAA VYA MIL 7/- HOSPITALI YA TEMEKE


SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) litatoa vifaa vyenye thamani ya sh. milioni 7.3 kwa Hospitali ya Temeke mkoani Dar es Salaam ambazo ni asilimia 5 ya fedha zilizopatikana kwenye mechi ya Simba na Azam.

Afisa habari wa TFF, Boniface Wambura amesema leo kuwa, mechi hiyo ya Ngao ya Jamii (Community Shield) kuashiria ufunguzi wa msimu mpya wa 2012/2013 ilichezwa juzi (Septemba 11 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kuingiza sh. 146, 640,000. Washabiki 26,001 walikata tiketi kushuhudia mechi hiyo ambayo ilimalizika kwa Simba kushinda mabao 3-2.

Alisema sekretarieti ya TFF inatarajia kukutana na uongozi wa Hospitali ya Temeke wakati wowote kuanzia leo ili kujua mahitaji halisi kabla ya kufanya ununuzi wa vifaa husika.

Wambura aliongeza kuwa mgawanyo wa mapato ya mechi hiyo uliokuwa kama ifuatavyo; asilimia 18 ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) sh. 22,368,813.56, asilimia 5 ya mchango wa kusaidia jamii (Hospitali ya Temeke) sh. 7,332,000, uwanja sh. 10,148,318.64, Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 4,059,327.46, TFF sh. 10,148,318.46 na Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 5,074,159.32.

Baraza la Michezo la Taifa (BMT) sh. 1,014,831.86, kila timu sh. 32,265,025.93, asilimia 10 ya gharama za mchezo sh. 10,148,318.64, nauli kwa waamuzi na kamishna sh. 80,000, posho ya kujikimu kwa waamuzi na kamishna 230,000, posho ya waamuzi 400,000, tiketi sh. 4,495,800, maandalizi ya uwanja (pitch) sh. 400,000, umeme sh. 300,000, usafi na ulinzi uwanjani sh. 2.350,000 na Wachina (Beijing Construction) sh. 2,000.000.

Alisema mchango wa kusaidia jamii kwenye mechi ya Ngao ya Jamii kuzindua msimu uliopita kati ya Yanga na Simba ulikuwa sh. 15,000,000 ambazo zilikwenda Chama cha Madaktari Wanawake Tanzania (MEWATA) kusaidia uchunguzi wa kansa ya matiti kwa akina mama.

No comments:

Post a Comment