Wednesday, September 19, 2012

SIMBA NI NOMA, YASHINDA LICHA YA KUBAKI 10 UWANJANI, YANGA HALI MBAYA MBAYA MBAYA

Wachezaji wa Moro United wakishangilia baada ya kufunga goli lao la kwanza


Kocha wa Yanga, Tom Saintfiet akishuhudia kipigo kwenye Uwanja wa Jamhuri leo

Wachezaji wa Yanga na Mtibwa wakiingia uwanjani

Wachezaji wa Mtibwa wakipita kuwapa mikono wachezaji wa Yanga kabla ya kuanza kwa mechi

Kikosi cha Mtibwa kilichotoa kipigo cha kukumbukwa kwa Yanga

Mashabiki wa Mtibwa wakishangilia bao la timu yao

Twende kule... mtu ambaye hakufahamika akichukuliwa na polisi


Foleni ya kuingia uwanjani Jamhuri mjini Morogoro

KUCHEZA wakiwa 10 uwanjani kwa zaidi ya dakika 50 hakukuwazuia mabingwa Simba kuchukua pointi tatu dhidi ya JKT Ruvu na kujiimarisha kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara kufuatia ushindi wa 2-0 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam leo, wakati mjini Morogoro mambo yalikuwa hovyo kwa Yanga baada ya kusambaratishwa kwa kipigo cha 3-0 kutoka kwa Mtibwa Sugar ugenini.


Azam, washindi wa pili wa mwaka jana walinyang'anywa tonge mdomoni katika dakika za majeruhi wakati walipolazimishwa sare ya 2-2 dhidi ya Toto African kwenye Uwanja wa CCM Kirumba baada ya kuongoza 2-1 kwa muda mrefu kupitia magoli ya Abdulhalim Humoud na Kipre Tchetche.

Simba walibaki 10 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam baada ya nyota wao Emmanuel Okwi kutolewa kwa kadi nyekundu ya moja kwa moja na refa Andrew Shamba katika dakika ya 38 kufuatia kumpiga kiwiko mchezaji wa JKT Kessy Mapande wakati matokeo yakiwa 0-0. Huenda Okwi akaikosa mechi dhidi ya mahasimu wao Yanga, Oktoba 3, kama atafungiwa kucheza mechi tatu, kama kanuni za kadi nyekundu ya moja kwa moja zinavyosema.


Mabingwa, licha ya kuwa pungufu, walijipanga na kupata magoli mawili kupitia kwa Amri Kiemba na Haruna Moshi 'Boban' na kufikisha pointi sita kutokana na mechi mbili.


Okwi alikuwa na nafasi ya mapema ya kuwapa Simba uongozi katika dakika ya 4, lakini akiwa tayari ameshawatoka mabeki wa JKT alipiga pembeni ya lango.  


Omary Changa alishindwa kufunga goli langoni mwa Simba akiwa amebaki yeye na kipa Juma Kaseja katika dakika ya 35 na dakika mbili baadaye Kaseja tena alipangua kiufundi shuti la Credo Mwaipopo.


Simba walikaribia kupata goli la kuongoza katika dakika ya 40, lakini shuti zuri la Boban liligonga mwamba na kurudi uwanjani.
Kiungo Kiemba aliipatia Simba goli lao kwanza katika dakika ya 46 akimalizia pasi ya Amir Maftah na Boban akaipatia Simba la pili katika dakika ya 63 kufuatia pasi ya Mrisho Ngassa.


Kocha wa Simba, Milovan Cirkovic alisema baada ya mechi hiyo kwamba amefurahi kupata pointi tatu lakini alimlalamikia mwamuzi kwa kadi nyekundu ya Okwi akisema hakustahili kutolewa, huku kocha wa JKT, Charles Kilinda akisema kwamba makosa ya kipa wao Shaban Dihile yalimkera ndio maana alimtoa na nafasi yake kuingia Said Mohammed katika dakika ya 78 wakiwa tayari wameshafungwa magoli mawili.


Kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro, ilikuwa ni aibu kubwa kwa mabingwa wa Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Yanga, ambao hawakuonyesha kama ni timu inayodhamiria kurejesha taji walilonyang'anywa na mahasimu wao Simba.


Mtibwa wangeweza kupata goli la kuongoza mapema katika dakika ya tano wakati Vincent Barnabas alipobaki yeye na kipa wa Yanga, Ali Mustapha 'Barthez', lakini mlinda-mlango huyo alipangua shuti na kuwa kona.


Mabeki wa Yanga walionekana kujichanganya na katika dakika 18 za kwanza tayari walikuwa wameshasababisha kona sita, ikiwamo iliyozaa bao la kuongoza la Mtibwa lilifungwa na Dickson Mbeikya katika dakika ya 13.


Hussein Javu aliiongezea Mtibwa goli la pili kwa shuti la umbali wa mita 17 baada ya mabeki wa Yanga, Kelvin Yondani na Mbuyu Twite kutegeana kuosha mpira uliokuwa jirani yao na kufanya matokeo yaliyobaki hadi mapumziko.


Javu tena akaipatia Mtibwa goli la tatu katika dakika 72 kwa shuti la mbali, ikiwa ni muda mfupi tu baada ya kipa wa zamani wa Yanga, Shabani Kado kupangua kiufundi shuti ya mtokea benchi Didier Kavumbagu aliyekuwa jirani na lango katika dakika ya 70.


Hamis Kiiza alithibitisha msemo "siku ya kufa nyani miti yote huteleza" pale alipokosa penalti kwa shuti lake kupaa juu ya lango katika dakika 89. Penalti hiyo ilitolewa na mwamuzi Mathew Akrama wa Mwanza baada ya beki wa kulia wa Mtibwa, Maliwa Ndeule 'kuunawa' mpira ndani ya boksi.


Kocha mpya wa Mtibwa na nahodha wa zamani wa Taifa Stars, Mecky Mexime, ambaye anafundisha timu ya wakubwa kwa mara ya kwanza ikiwa ni miaka michache baada ya kustaafu soka, aliwashukuru wachezaji wake baada ya mechi hiyo, lakini alisema ni lazima wayasahau matokeo hayo haraka kwani kuifunga Yanga peke yake hakutoshi kuwapa mafanikio katika ligi.


Kocha wa Yanga, Mbelgiji Tom Saintfiet, ambaye juzi alikaririwa akilalamikia maandalizi mabovu kwa upande wa menejimenti ya timu baada ya wachezaji wake kulazwa wawili wawili katika vitanda vyembamba vya hoteli "iliyochoka", aliingia mitini baada ya mechi.


Mkoani Mbeya kuwa, Prison walilazimisha sare ya pili mfululizo baada ya kutoka 1-1 dhidi ya Coastal Union ya Tanga kwenye Uwanja wa Sokoine.


Coastal ambao walianza msimu kwa kuifunga Mgambo JKT 1-0 kwenye Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga Jumamosi, leo walipata goli la kuongoza katika dakika ya 30 kupitia kwa kiungo wa zamani wa Simba, Jerry Santo, kabla ya wenyeji ambao katika mechi ya awali waliishikilia Yanga katika sare ya 0-0, kusawazisha katika dakika ya 52 kupitia kwa Fred Chudu.


Katika mechi iliyochezwa Mlandizi, mkoani Pwani, Ruvu Shooting walishinda 2-1 dhidi ya wageni wa ligi hiyo Mgambo JKT ya Tanga. Zilikuwa ni pointi tatu za kwanza kwa Shooting ambao walilala 2-1 dhidi ya JKT Ruvu Jumamosi na kipigo cha pili mfululizo kwa Mgambo.


Kwenye Uwanja wa Chamazi jijini Dar es Salaam, African Lyon ilizinduka kutoka kwenye kipigo cha 3-0 kutoka kwa Simba Jumamosi na kushinda 1-0 dhidi ya Polisi Moro ambayo ilianza msimu kwa sare ya 0-0 dhidi ya Mtibwa Jumamosi.


Kagera Sugar ilipata pointi yake ya kwanza kufuatia sare ya 0-0 dhidi ya JKT Oljoro kwenye Uwanja wa Kaitaba. Katika mechi ya kwanza Kagera Sugar ilichapwa 1-0 na Azam kwenye uwanja wao huo wa nyumbani.


Vikosi kwenye Uwanja wa Taifa; Simba: Juma Kaseja, Nassoro Said 'Chollo', Amir Maftah, Shomari Kapombe, Juma Nyosso, Amri Kiemba, Mwinyi Kazimoto, Haruna Moshi 'Boban', Daniel Akuffor/ Ramadhani Chombo 'Redondo' (dk.61), Mrisho Ngassa/ Abdallah Juma (dk.81) na Emmanuel Okwi
JKT Ruvu: Shaban Dihile/ Said Mohammed (dk.78), Kessy Mapande, Stanley Nkomola, Damas Makwaya, George Minja, Ally Khan, Said Otega/ Amos Mgisa (dk.53), Jimmy Shoji, Omary Changa, Hussein Bunu na Credo Mwaipopo.


Vikosi kwenye Uwanja wa Jamhuri; Yanga: Ali Mustapha 'Barthez', Juma Abdul, Mbuyu Twite/ Didier Kavumbagu (dk.64), Nadir Haroub 'Cannavaro', Kelvin Yondani, Athumani Idd 'Chuji', Frank Domayo/ Simon Msuva (dk.46), Haruna Niyonzima, Said Bahanunzi, Hamisi Kiiza na David Luhende/ Stephano Mwasika (dk.46).


Mtibwa: Shaban Kado, Maliwa Ndeule, Issa Rashid, Dickson Mbeikya, Salvatory Ntebe, Shaban Nditi, Jamal Mnyate, Awadhi Juma, Hussein Javu, Shaban Kisiga na Vincent Barnabas/ Ally Mohammed (dk.63).

MATOKEO YOTE MECHI ZA LIGI KUU YA BARA LEO


JKT Ruvu             0-2 Simba

Mtibwa Sugar        3-0 Yanga

African Lyon        1-0 Polisi Moro

Ruvu Shooting      2-1 Mgambo JKT

Tanzania Prisons   1-1 Coastal Union

Kagera Sugar        0-0 JKT Oljoro

Toto Africans        2-2 Azam 


 Msimamo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara:
                                    P      W  D    L   GF   GA    GD    Pts
1.Simba                       2      2    -     -    5       -         5        6    
2.Mtibwa Sugar         2      1    1    -    3       -         3        4
3. Coastal Union        2      1    1    -    2       1         1        4
4.Azam FC                 2       1    1    -   2       1         1        4
5.Ruvu Shooting        2      1     -    1   3      3          -         3
6.JKT Ruvu               2      1     -    1   2       3        -1        3
7.African Lyon          2      1     -    1   1       3       -2        3
8.Tanzania Prisons    2      -     2   -    1       1         -        2
9. Toto Africa            2       -    2   -    2       2         -         2
10. Police Oljoro       2       -    2   -    1      1          -        2
11.Police Moro          2       -    1   1   -       1         -1       1
12.Kagera Sugar       2       -    1   1   -       1         -1       1
13.Yanga                    2       -    1   1   -      3          -3       1
14. Mgambo JKT      2       -    -    2   -      3         -2        -

No comments:

Post a Comment