Thursday, September 20, 2012

DIAMOND: NATAKA KUTENGENEZA AJIRA KWA VIJANA WENZANGU


MSANII wa kimataifa wa Tanzania, Naseeb Abdul a.k.a Diamond Platnumz amesema amedhamiria kutoa ajira kwa vijana wengi wa Kitanzania kupitia muziki huku pia akileta mapinduzi katika sekta hiyo nchini.

Diamond ambaye ni msanii ghali zaidi kwa sasa Tanzania, amesema kuna watu wengi wenye vipaji ambao wako mtaani au wako katika sekta nyingine lakini hawajui wafanyeje ili kufikia ndoto zao jambo ambalo linahitaji watu wengine wawasaidie kuwafikisha pale wanapotaka.

“Kuna tatizo ambalo lipo katika mambo ya mitindo, muziki. Watu wengi wanachukulia kama uhuni, wengi wanaona kama kuuza sura, yaani mtu aonekane kwenye video ili apate umaarufu, tunatakiwa kubadilisha mawazo haya, Ulaya hata hapo Afrika Kusini wanaonekana kwenye video wanalipwa.

“Mimi nitawalipa wote watakaoonekana kwenye video yangu, tutakapofanya usaili Jumamosi (kesho) wale watakaochanguliwa watalipwa, lakini pia hii inaweza kuwa ni kufunguliwa milango kwenye sekta nyingine, wapo wanaoweza kuonekana wanafaa kwenye matangazo ya biashara, hawa watapata kampuni ambazo zinaweza kuwatumia.

“Katika majaji watakuwepo Raqey Mohammed wa I-View Studios, hawa wanafanya kazi nyingi za matangazo, filamu, atakuwepo pia Ally Rehmtullah huyu ni mbunifu anayeweza kumuona mtu na akasema huyu anafaa kwa sekta yake, Sammy Cool ni densa na mwalimu hata Missie Popular yeye ni mwandishi na mwanamitindo wanajua wapi kwa kuwafikisha watu wengine," alisema.

Msanii huyo alisema mafanikio aliyo nayo ya kumiliki nyumba, magari na kujulikana kwake yametokana na muziki, hivyo ana uhakika wapo watu wengine pia kupitia yeye na wanamuziki wengine kama yeye wanaweza kufaidika na kufikia mafanikio kama aliyoyapata.

Diamond alisema usaili huo unafanyika kesho pale kwenye ukumbi wa Nyumbani Lounge kuanzia saa tano asubuhi. Hii ni mara ya kwanza kwa msanii wa nchini kufanya usaili kwa ajili ya watu watakaonekana kwenye video yake.

Diamond pia ndiye msanii wa kwanza wa muziki wa kizazi kipya kuandaa shoo yake mwenyewe na watu kulipa kiingilio cha Sh. 50,000. Diamond alifanya hivyo kwenye onyesho alilolipa jina la Diamond are Forever pale Mlimani City, Dar es Salaam na alikaririwa akisema kwamba onyesho hilo lilimuingizia Sh. milioni 100.

No comments:

Post a Comment