Thursday, September 20, 2012

SARE NA JUVE YAMCHANGANYA KOCHA DI MATTEO CHELSEA

Kocha wa Chelsea, Roberto di Matteo
Mfungaji wa bao pekee na la ushindi la Manchester United, Michael Carrick akipiga makofi baada ya mechi yao ya Kundi H la Ligi ya Klabu Bingwa dhidi ya Galatasaray kwenye Uwanja wa Old Trafford mjini Manchester jana Septemba 19, 2012. Man U ilishinda 1-0. Picha: REUTERS

KOCHA Roberto Di Matteo alisema Chelsea iliachwa imechanganyikiwa baada ya kupoteza uongozi wa 2-0 dhidi ya Juventus katika mechi yao ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya iliyoisha kwa sare ya 2-2, lakini alimsifu Oscar kwa kufunga magoli mawili katika mechi yake ya kwanza kuanza.

Mbrazili huyo alifunga magoli mawili ndani ya dakika mbili kabla ya Juve kujibu mapigo kupitia kwa Arturo Vidal na Fabio Quagliarella, ambaye alisawazisha zikiwa zimebaki dakika 10.

"Tumefadhaishwa na imetuchanganya kiasi," alisema Di Matteo.

"Oscar alifanya kazi nzuri kiufundi na kufunga magoli mawili."

Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 21, ambaye alijiunga akitokea katika klabu ya Internacional ya Brazil kwa ada ya uhamisho ya paundi milioni 25 katika kipindi kilichopita cha usajili, alifunga goli lake la kwanza kwa Chelsea kwa shuti lililomgonga beki na kubadilishwa mwelekeo, kabla ya kufunga goli bab'kubwa kutokea nje ya boksi.

Kiungo wa ulinzi, John Obi Mikel alipoteza mpira katika shambulizi la goli la kusawazisha, na akakamilisha makosa yake kwa kushindwa kumzuia Claudio Marchisio asimpasie Quagliarella.

"Kama natafuta kisingizio, naweza kupata," mchezaji huyo wa kimataifa wa Nigeria alisema. "Lakini, kwangu, nilipoteza mpira. Naweka mikono juu, tuendelee mbele.

"Samahani kwa kosa nililofanya, lakini hakuna visingizio. Nadhani kile ndicho kitu unachopata unapocheza kwenye Ligi ya Klabu Bingwa.

"Ukifanya kosa, unaadhibiwa."

Mechi inayofuata ya Chelsea itakuwa ni dhidi ya klabu ya Denmark ya FC Nordsjaelland, ambayo ilianza kwa kufungwa 2-0 na Shakhtar Donetsk katika mechi yao ya ufunguzi ya Kundi E, katika mechi yao ya pili ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya Jumanne ya Oktoba 2.

No comments:

Post a Comment