Saturday, September 15, 2012

RONALDO: MESSI NI MKALI ZAIDI YA CRISTIANO RONALDO

Ronaldo de Lima
Lionel Messi wa FC Barcelona (kushoto) akiwafungasha tela Tino Costa (katikati) na Adil Rami wa Valencia wakati wa mechi yao ya La Liga kwenye Uwanja wa Camp Nou mjini Barcelona, Hispania Septemba 2, 2012.

Cristiano Ronaldo

STRAIKA wa zamani wa Real Madrid, Ronaldo de Lima anaona kwamba nyota wa Barcelona, Lionel Messi ni bora kidogo zaidi ya straika wa Real Madrid, Cristiano Ronaldo, kwa sababu ni mbunifu zaidi uwanjani.

Nyota hao wawili wa Ligi Kuu ya Hispania wanaaminika kwa wengi kuwa ndo wanasoka bora zaidi duniani kwa sasa, na Ronaldo anaona Muargentina Messi ni zaidi huku akielezea jinsi anavyomkubali Mreno Ronaldo.

"Messi yuko juu kidogo ya Cristiano Ronaldo kwa mtazamo wangu," nyota huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Brazil alikaririwa na CNN akisema.

"Namkubali zaidi Messi, kwa sababu yeye ni mchezaji anayetukosha zaidi, ambaye anaonyesha ubunifu zaidi - licha ya kwamba anatokea Argentina, ambao ni mahasimu wakubwa wa nchi yangu Brazil.

"Nawakubali wote, hata hivyo."

Gwiji huyo mwenye umri wa miaka 35 pia akazungumzia hatma ya yosso wa Brazil, Neymar, na akasema anahitaji kwenda Ulaya ili kupiga hatua moja mbele.

"Nadhani Neymar ana kazi ya kukamilisha, kucheza Ulaya na kutwaa mataji akiwa Ulaya."

Ronaldo anasubiri kwa hamu fainali za Kombe la Dunia 2014 zitakazofanyika kwao Brazil, na licha ya kwamba timu yao ya taifa maarufu pia kama "Selecao" haijaonyesha kiwango katika miaka ya karibuni, straika huyo wa zamani ana matumaini kwamba wanaweza kupigania ubingwa ndani ya miaka miwili ijayo.

"Nadhani katika mataji mawili ya mwisho tuliyotwaa ya Kombe la Dunia (1994 na 2002), timu ilikuwa ikipikwa mwaka mmoja tu nyuma. Hivyo nadhani bado tunao muda," aliongeza.

"Tunaye Neymar, ambaye ana kipaji kikubwa, Pato, Thiago Silva, ambaye ni beki mwengine mkali. Ganso, Oscar. Tuna timu ya vijana, lakini wanacheza katika kiwango cha juu na hilo linatupa matumaini ya ubingwa."

Brazil walitolewa katika robo-fainali katika fainali zote za Kombe la Dunia za mwaka 2006 na 2010.

No comments:

Post a Comment