Tuesday, September 25, 2012

REFA ALIYEMTOA SHELVEY KWA NYEKUNDU AOMBEWA KIFO KWA KANSA, ATISHIWA MAISHA, AKIMBILIA POLISI

Refa Mark Halsey (kulia) akimtoa Shelvey kwa kadi nyekundu

REFA Mark Halsey amepokea vitisho na matusi na amekimbilia polisi kushitaki.

Halsey ametukanwa na kuombewa arejewe na ugonjwa wake wa kansa na afe baada ya kumtoa Jonjo Shelvey kwa kadi nyekundu na kuwapa Manchester United penalti ya utata katika ushindi wa 2-1 dhidi ya Liverpool kwenye Uwanja wa Anfield Jumapili.

Matusi aliyopokea yamepingwa na chama cha marefa ambacho kimesema yamepita kipimo na kwamba wako tayari kutoa msaada wowote utakaohitajika.

Halsey, ambaye aliugua ugonjwa wa saratani ya koo mwaka 2009 lakini akarejea kufanya kazi ya urefa Machi 2010 baada ya kutibiwa kimafanikio, alimuonyesha Shelvey kadi nyekundu kwa tukio la kuwania mpira dhidi ya Jonny Evans na akawapa Manchester United penalti ya dakika za lala salama ambayo Robin van Persie alifunga na kuwapa ushindi wa 2-1.

Ujumbe wa Twitter uliotumwa kwa akaunti ya @johnwareing1 ulisomeka: "Natumai Mark Halsey atapata kansa tena na afe", wakati ujumbe mwingine kutoka kwa @lfcjohn259 ulisomeka: "Mark Halsey ni bora angekufa kwa kansa."

Ujumbe huo wa kwenye Twitter uliibua hasira kwenye mitandao ya kijamii na yote iliondolewa haraka.

Mke wa Halsey, Michelle, pia alipata meseji za matusi. Ripoti zinadai kuwa "chama" cha marefa, Professional Game Match Officials Ltd (PGMOL), kitampa Halsey fursa ya kuonana na mshauri nasaha kama atahitaji, lakini anatarajiwa kuchezesha mechi ya Kombe la Capital One baina ya Southampton na Sheffield Wednesday leo kama ilivyopangwa.

No comments:

Post a Comment