Sunday, September 30, 2012

NIZAR KHALFANI AANZA MAMBO YANGA IKIUA LYON 3-1

Mshambuliaji wa Yanga, Simon Msuva (kulia) akitafuta mbinu za kumtoka mlinzi wa African Lyon, Sunday Bakari wakati wa mechi yao ya ligi kuu soka Tanzania bara kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam leo. Yanga ilishinda 3-1.

NIZAR Khalfani alifunga magoli mawili na Nadir Haroub 'Cannavaro' akaongeza moja wakati Yanga iliposhinda 3-1 mbele ya kocha wao mpya Mholanzi Ernie Brandts aliyekuwa jukwaani kutokana na kukosa kibali cha kazi na kuipa African Lyon kipigo cha tatu katika mechi nne za ligi kuu ya Bara kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam leo.


Nizar aliyeingia katika dakika ya 61 kuchukua nafasi ya Frank Domayo, alihitaji dakika 2 tu uwanjani kuandika goli lake la kwanza na la pili kwa timu yake katika dakika ya 63 akiunganisha kwa kichwa krosi ya Simon Msuva na akaifungia Yanga la tatu katika dakika ya 88 akiuwahi mpira wa 'tik-taka' ya Said Bahanunzi iliyogonga 'besela' na kuangukia mbele ya lango.


Yanga ndiyo waliotangulia kwa goli la mapema katika dakika ya 16 kupitia kwa beki wa kati Cannavaro aliyepanda mbele kusaidia mashambulizi na kufunga kirahisi kufuatia pasi ya kupenyezewa huku mabeki wakidhani ameotea.


Licha ya kutawala mechi kwa muda mwingi kufikia kukaa na mpira kwa asilimia 65 dhidi ya 35 za Lyon, Yanga walifungwa goli la shambulizi la kustukiza katika dakika ya 62 kupitia kwa Benedictor Mwamlangala kufuatia pasi tamu ya Jacob Masawe.


Sherehe kubwa za mno za kushangilia goli hilo zilizoonekana hata kwa kocha wao Muargentina Baplo Ignasio Velez aliyekuwa kama "kapagawa" kwa kusawazisha, ziliwagharimu Lyon, ambao walijikuta wakifungwa goli la pili kwa shambulizi la moja kwa moja baada ya Yanga kuanza mpira cha katikati ya uwanja.


Pasi ndefu ya kuelekea kwenye wingi ya kushoto ilimkuta Msuva aliyemimina krosi katikati na kutua kichwani mwa Nizar aliyefunga goli lake la kwanza kwenye ligi kuu tangu aliporejea nchini akitokea Marekani alikokuwa akicheza soka la kulipwa na akaongeza lake la pili dakika mbili kabla ya firimbi ya mwisho.


Kocha wa muda, Fred Minziro, aliyeiongoza Yanga katika mechi mbili alizoshinda zote tangu kufukuzwa kwa kocha wao Mbelgiji Tom Saintfiet, alisema baada ya mechi hiyo kwamba licha ya ushindi, timu yake ilipoteza nafasi nyingi za kufunga na ingeweza kupata matokeo mazuri zaidi ya hayo.


Alisema akili zao sasa wameziweka katika mechi kubwa ya Jumatano dhidi ya mahasimu wao Simba na kwamba wachezaji wake watarejea wakiwa wapya zaidi kiufundi. Katika mechi iliyopita baina ya timu hizo zenye upinzani wa jadi, Yanga ilikumbana na kipigo cha aibu cha 5-0.


Vikosi vilikuwa; 

Yanga:
Ali Mustapha 'Barthez', Mbuyu Twite, Oscar Joshua/ Stephano Mwasika (dk.88), Kelvin Yondani, Nadir Haroub 'Cannavaro', Athuman Idd 'Chuji', Frank Domayo/ Nizar Khalfan (dk. 61), Frank Domayo, Didier Kavumbagu, Hamis Kiiza/ Said Bahanunzi (dk.58) na Haruna Niyonzima.
 

African Lyon:
Abdul Seif, Omar Mtaki, Hamad Manzi, Sunday Bakari/ Idd Mbaga (dk.78), Benedictor Mwamlangala/ Fred Lewis (65), Robert Mkotya/ Semmy Kessy (dk. 50), Obina Salamusasa, Mohamed Samata, Hood Mayanja, Jacob Masawe na Yusuf Mlipili.

Msimamo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya mechi ya leo:
                                 P        W      D     L    GF          GA          GD        Pts
1.Simba                     4         4       -        -        9           2              7         12   
2.Azam FC               4         3       1        -       7           2              5          10
3.JKT Oljoro              4         2       2        -       6           2              4          8
4.Coastal Union        4         2       2        -        3           1              2           8
5.Yanga                    4         2       1        1       7           5              2          7
6.Tanzania Prisons    4         1       2         1        4           4               -          5
7. Mtibwa Sugar      3         1       1         1       3            1              2           4

8.Toto Africa            4         -       4         -        2            2              -            4
9.Kagera Sugar        4        1       1         2       1            2            -1           4
10.Ruvu Shooting     3        1       -         2       4            5             -1           3
11.African Lyon        4       1       -         3       3           8             -5            3
12.JKT Ruvu           4        1       -         3       3           10            -7           3
13.Police Moro        4       -        2        2        -            2             -2           2
14. Mgambo JKT    4        -        -        4        2            7             -5           -

No comments:

Post a Comment