Sunday, September 30, 2012

ANZHI MAKHACHKHALA YA SAMUEL ETO'O YATHIBITISHA KWELI MPIRA PESA ... ETO'O ATUPIA MOJA NA KUTENGENEZA JINGINE WAKATI WAKIIBUKA NA USHINDI WA 2-1 NA KUKWEA KILELENI MWA MSIMAMO WA LIGI KUU YA URUSI... WAWADUWAZA VIGOGO CSKA MOSCOW NA ZENIT YA MBRAZIL HULK...!

Samuel Eto'o aki[pongezwa na wachezaji wenzake wa Anzhi baada ya kufunga goli.
Samuel Eto'o akishangilia baada ya kufunga goli wakati wa mechi yao ya Ligi Kuu ya Urusi.
Samuel Eto'o akishangilia baada ya kumalizika kwa mechi yao ya Ligi Kuu ya Urusi dhidi ya Volga Nizhny Novgorod leo.

Tunatishaaaaa....! Samuel Eto'o akipongezwa na wenzake baada ya kufunga goli moja na kutengeneza jingine wakati wakishinda 2-1 dhidi ya Volga Nizhny Novgorod katika mechi yao ya Ligi Kuu ya Urusi leo.
MOSCOW, Urusi
Samuel Eto'o na Lacina Traore kila mmoja alifunga goli moja na kuipaisha klabu tajiri ya Anzhi Makhachkala kukwea kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya Urusi leo baada ya kuibuka na ushindi wa 2-1 dhidi ya Volga Nizhny Novgorod.

Straika wa kimataifa wa Cameroon, Eto'o alifunga goli lautangulizi kwa shuti safi muda mfupi kabla ya mapumziko, akitumia 'pande' safi alilopewa na mchezaji wa kimataifa wa Ivory Coast, Traore.

Eto'o, aliyejiunga na mabilionea wa Anzhi akitokea Inter Milan Septemba mwaka jana, alirudisha fadhila katika dakika ya 62 baada ya kumtengenezea pasi safi Traore aliyefunga bao la ushindi ikiwa ni dakika tatu baada ya Volga kusawazisha.

Ushindi huo wa tano mfululizo uliipaisha Anzhi, inayoongozwa na kocha wa zamani wa timu ya taifa ya Urusi, Guus Hiddink, ikiwa na pointi mbili zaidi ya vinara wa awali, CSKA Moscow, ambao walichapwa 2-0 mapema leo katika mechi yao dhidi ya mahasimu wao wa jadi, Dynamo.

"Leo tulikuwa na hamasa ya ziada ya kushinda kwa sababu tulijua kwamba CSKA tayari wameshapoteza mechi yao," Mholanzi Hiddink, aliyeifikisha Urusi katika hatua ya nusu fainali ya Euro 2008, aliwaambia waandishi wa habari.

"Sasa tuko kileleni mwa msimamo wa ligi ngumu ya Urusi. Hii ni hatua kubwa kwa klabu yetu."

Kwa ushindi wao, Anzhi pia wamewaacha kwa pointi tano vigogo wengine, Zenit St. Petersburg, ambao wanakamata nafasi ya saba kwenye msimamo wa ligi hiyo licha ya kutumia zaidi ya Euro milioni 100 (Sh. bilioni 200) kusajili nyota kadhaa mwanzoni mwa msimu huu akiwamo Mbrazili Hulk. Lokomotiv sasa wanakamata nafasi ya tatu, wakizidiwa kwa pointi moja na CSKA wanaokamata nafasi ya pili.

Mbali na Eto'o, Anzhi inayosifika kwa kulipa mishahara minono wachezaji wake inaundwa pia na Lassana Diarra aliyetua msimu huu akitokea Real Madrid na Christopher Samba aliyetua msimu uliopita akitokea Balckburn Rovers.

No comments:

Post a Comment