Tuesday, September 25, 2012

NEMANJA VIDIC APASULIWA GOTI... KUWA NJE YA KIKOSI CHAKE CHA MANCHESTER UNITED KWA MIEZI MIWILI

Nemanja Vidic

LONDON, England
Nahodha wa Manchester United, Nemanja Vidic atakuwa nje ya kikosi cha timu yake kwa miezi miwili baada ya kufanyiwa upasuaji wa goti, klabu hiyo ya Ligi Kuu ya England imesema leo.

Beki huyo wa kimataifa wa Serbia, alikuwa nje kwa miezi sita msimu uliopita kutokana na jeraha la goti kabla ya kurejea katika kikosi cha kwanza mwanzoni mwa msimu huu.

"Nemanja Vidic amefanyiwa upasuaji wa goti lake la kulia na atakuwa nje kwa takriban wiki nane," Man U imesema leo katika taarifa yake kupitia tovuti yao rasmi (www.manutd.com).

"Sir Alex (Ferguson), kwa tahadhari, alimpumzisha Vidic mwishoni mwa wiki, baada ya kulalamikia maumivu ya goti, hata hivyo, uchunguzi zaidi wa kitaalam umebaini tatizo lake.

"Beki huyo wa kati alipasuliwa wiki hii na atakuwa nje kwa wiki nane."

Kukosekana kwa beki huyo mwenye miaka 30 ni pigo jingine kubwa kwa Ferguson, ambaye tayari alishawakosa mabeki Phil Jones na Chris Smalling wanaosumbuliwa na majeraha.

Man U wameshinda mechi nne katika mechi zao tano za mwanzo wa msimu wa Ligi Kuu ya England lakini wameonekana kuyumba katika safu yao ya mabeki, huku Rio Ferdinand na Jonny Evans wakiwa ndio wachezaji pekee wazoefu  kwa nafasi ya ulinzi wa kati walio 'fiti' kucheza.

No comments:

Post a Comment