Ronaldo akiugulia 'enka' jana |
Mmhh... timu yangu sasa kweli kimeo! Mourinho anavyoonekana kabla ya kuanza mechi yao jana dhidi ya Sevilla. |
Tumekwisha...! Mourinho (kushoto) na wenzake katika benchi la Real Madrid wakionekana wapole wakati dakika zikiyoyoma huku wakiwa nyuma kwa bao 1-0 katika mechi yao dhidi ya Sevilla jana. |
Lionel Messi wa Barcelona akipiga penati na kufunga dhidi ya Getafe wakati wa mechi yao ya La Liga kwenye Uwanja wa Coliseum Alfonso Perez mjini Getafe, janaSeptemba 15, 2012. (Picha: REUTERS) |
Tunatishaaa...! David Villa wa Barcelona akishangilia goli alilofunga dhidi ya Getafe jana. |
Kocha Jose Mourinho amekiponda kikosi chake cha Real Madrid baada ya kukubali kipigo cha ugenini cha bao 1-0 kutoka kwa Sevilla jana usiku, akidai kwamba kiwango kibovu cha wachezaji wake ndicho kilichowaponza.
Real Madrid wameanza na rekodi mbaya kabisa katika La Liga, Ligi Kuu ya Hispania msimu huu, wakiambulia pointi nne tu katika mechi walizocheza, ambazo zimewaweka miongoni katika kundi la "wachovu" kwenye msimamo wa ligi baada ya kuangukia katika nafasi ya 10, na pia wameachwa kwa pointi nane na vinara Barcelona ambao ni mahasimu wao wa jadi.
Mourinho amesisitiza kwamba hajafurahishwa na kiwango cha wachezaji, na anaamini kwamba bado hawajarekebisha makosa waliyoonyesha tangu mwanzo wa msimu huu.
“Hivi sasa, sina timu kwakweli," Mourinho amewaambia waandishi wa habari baada ya mechi kumalizika. "Kipindi cha kwanza na pia kipindi cha pili, hatukucheza vizuri. Kwakweli ni ushindi uliostahili kwenda kwa Sevilla na pia ni kipigo cha haki kwa Real Madrid.
"Hongera kwa Sevilla kwa sababu walifanya kila walilotakiwa ili kushinda na wamepata ushindi walioustahili pasi na shaka yoyote ile. Tulistahili kipigo katika mechi hii.
"Mechi ya leo (jana) haikuwa tofauti na ile dhidi ya Getafe. Haina tofauti vilevile na tulivyocheza dhidi ya Granada, licha ya kwamba hiyo tulishinda. Sidhani kama matokeo haya yanahusiana na uvumi uliotanda katika wiki mbili zilizopita.
"Kwangu mimi, ni kwa sababu ya sisi wenyewe kwa pamoja kama timu."
"Kuna wachezaji wachache waliocheza vizuri na kujituma, na ambao inaonekana kwamba mpira kwao ndio kitu muhimu na ni sehemu ya maisha yao. Wakati unapokuwa na watu ambao hawajitumi, inakuwa ngumu.
"Lakini mimi ndiye kocha, hivyo kama kuna watu hawajitumi, ni kosa langu."
Mourinho alijizuia kidogo 'kuwaua' sana wachezaji wake hata hivyo kulinganisha na vile alivyowaponda baada ya mechi waliyopigwa 2-1 dhidi ya Getafe.
"Wakati wa mapumziko, nilibadili wachezaji wawili, lakini nilitamani kuwatoa wachezaji saba," aliongeza.
"Muonekano wa timu yangu hivi sasa ni kwamba, ni timu iliyokosa umakini, isiyo na morari wa kujituma. Wakati unapoilinganisha Real na Sevilla unaelewa hili kirahisi.
"Kwa Sevilla, kila mpira ulikuwa ni kitu cha mwisho kwao katika maisha. Walipambana kwa ukamilifu katika kila kitu. Walitaka kucheza kwa kasi, kupeleka mpira haraka.
"Timu yangu ilifanya hivyo dhidi ya Barcelona, na haijafanya hivyo tena katika mechi nyingine."
Real Madrid watacheza dhidi ya Manchester City Jumanne usiku katika mechi yao ya ufunguzi wa Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya.
Wakati vijana wa Mourinho wakiendelea 'kumbwela-mbwela' katika msimamo wa La Liga, mahasimu wao Barca walijichimbia kileleni baada ya kufikisha pointi 12 kufuatia ushindi wao dhidi ya Getafe, pointi mbili zaidi ya Malaga wanaoendelea kushika nafasi ya pili baada ya kushinda pia jana kwa mabao 3-1 dhidi ya Levante. Sevilla walikwea hadi katika nafasi ya tatu baada ya kufikisha pointi nane.
Katika mechi nyingine, Valencia walishinda 2-1 dhidi ya Celta Vigo.
No comments:
Post a Comment