Sunday, September 16, 2012

REAL MADRID YAPIGWA TENA, BARCA YAUA, MESSI ATUPIA 2, RONALDO HOI

Messi (wa pili kulia) akishangilia pamoja na David Villa (kulia) na Pedro (kushoto)

REAL Madrid walikumbana na kipigo chao cha pili katika mechi nne za kwanza za Ligi Kuu ya Hispania wakati walipolala 1-0 ugenini dhidi ya Sevilla, huku mahasimu wao Barcelona wakizidi kupaa kileleni mwa msimamo kwa ushindi wa nne mfululizo baada ya kuichakaza Getafe 4-1.

Kipigo hicho cha pili mfululizo kwa Real kinamaanisha kwamba mabingwa hao wa La Liga wameachwa kwa pointi nane tayari katika mechi nne tu za kwanza za msimu.

Piotr Trochowski alifunga kwa shuti lililotinga darini mwa lango la Real katika sekunde ya 69 kufuatia uzembe wa mabeki kushinda kumpa ulinzi na kumfanya akiunganisha peke yake mpira wa kona muda mfupu baada ya mpira kuanza.

Real hawakuweza kujibu mapigo hayo na badala yake wanapaswa kujihesabu wenye bahati kwamba wachezaji wao wawili wangeweza kirahisi kabisa kutolewa kwa kadi nyekundu huku wakikoswa maholi mengi ya wazi.

Kocha wa Real, Jose Mourinho aliulizwa kuhusu tofauti ya pointi nane katika msimamo wa ligi baada ya kucheza mechi zao nne: "Naihofia timu yangu na hiyo ni kwa sababu tangu mwanzo wa msimu tumecheza vizuri mechi ya Super Cup, afadhali kidogo dhidi ya Valencia na kidogo dhidi ya Granada.

"Hiyo ndiyo hofu yangu kuliko pointi. Kwa sasa sina timu."

Kocha wa Barcelona, Tito Vilanova alimsifu Lionel Messi baada ya kuingia kipindi cha pili akitokea benchi na kufunga magoli mawili dhidi ya Getafe. Magoli mengine yalifungwa na beki Adriano na mtokea benchi mwingine David Villa.

Vilanova alisema: "Nilizungumza naye. Amefanya kazi kwa bidii kwa kipindi chote cha kujiandaa na msimu na ametoka kucheza mechi ngumu. Alikuja katika mechi ya leo baada ya safari ndefu akiwa ameichezea mechi kadhaa timu yake ya taifa. Niliamua kuwachezesha wachezaji waliopumzika na kumuingiza Messi wakati mechi ikiwa ni ya wazi zaidi."

No comments:

Post a Comment