Wednesday, September 12, 2012

MGONGOLWA AKANUSHA KELVIN YONDANI KUHALALISHWA YANGA KUPITIA KURA... ATOA UFAFANUZI WA KINA KUHUSU KANUNI ILIYOMPELEKA BEKI HUYO KWA 'WANAJANGWANI'

Kelvin Yondani
MWENYEKITI wa Kamti ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji, Alex Mgongolwa amesisitiza kuwa beki Kelvin Yondani ni halali kuichezea Yanga na kukanusha taarifa zilizodai kuwa wajumbe wa kamati yake walilazimika kupiga kura ili kufikia uamuzi huo.

Mgongolwa ametoa ufafanuzi huo wakati akihojiwa jana, akisisitiza kuwa Yanga walimsajili kihalali Yondani kutoka Simba kwa kuzingatia ibara ya 44(3) ya Kanuni za Uhamisho wa Wachezaji za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na pia ibara ya 18(3) ya kanuni za uhamisho wa wachezaji za Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).

"Si kweli... masuala ya kanuni hayahitaji upigaji kura," alisema Mgongolwa wakati alipoulizwa kuhusu taarifa zilizozagaa juzi na kuripotiwa jana na vyombo vya habari kuwa wajumbe wa kamati yake walilazimika kupiga kura ili kuhalalisha uhamisho wa Yondani kwenda Yanga.

Akifafanua zaidi, Mgongolwa alisema kuwa ibara ya 44(3) inaeleza wazi kwamba mchezaji anaweza kusajiliwa na klabu nyingine kwa namna tatu, ikiwamo ya klabu inayomtaka kuzungumza na klabu inayommiliki ili kupata ridhaa yao na ndipo wamalizane na mchezaji husika.

Mgongolwa aliitaja njia nyingine kuwa ni kuzungumza na mchezaji mwenyewe moja kwa moja, lakini kwa sharti kwamba mkataba wake (mchezaji) na klabu yake ya awali uwe umemalizika na kwamba hapo, klabu inayomhitaji mchezaji wa aina hiyo haitalazimika kuzungumza na timu yake ya awali ili kupata idhini ya kumsajili.
Mwenyekiti huyo aliitaja njia ya tatu kuwa ni ya klabu kuzungumza pia na mchezaji mwenyewe moja kwa moja bila kuhitaji ruhusa ya timu yake ya awali kwa sharti kwamba kipindi kilichobaki kabla ya kumalizika kwa mkataba wa awali (baina ya mchezaji na timu yake ya awali) kuwa miezi sita au chini ya kipindi hicho.

Mgongolwa alisema kuwa baada ya kufuata njia mojawapo kati ya hizo, klabu na mchezaji hutakiwa kuwasilisha mkataba wao kwa shirikisho (TFF) ili usajiliwe na kwamba wasipofanya hivyo, mkataba wao hautatambuliwa.

Alisema kuwa Yanga walimalizana na Yondani na kuusajili mkataba walioingia naye Mei 12, 2012; ikiwa ni kipindi cha chini ya wiki tatu kabla ya kumalizika kwa mkataba wa awali wa mchezaji huyo (Yondani) na klabu yake ya zamani ya Simba uliomalizika wiki tatu baadaye (Mei 31, 2012).

Aliongeza kuwa wakati Yanga wakisajili mkataba wao na Yondani kwenye ofisi za TFF, Simba hawakuwa na mkataba wowote mpya waliousajili kabla ya terehe hiyo (Mei 12, 2012), jambo linalompa uhalali beki huyo anayeichezea pia timu ya taifa (Taifa Stars) kuvaa 'uzi' wa Yanga msimu ujao.

Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage alikaririwa jana akipinga maamuzi ya kamati ya Mgongolwa (ambayo naye ni mjumbe)  huku akidai kwamba kura zilitumika kumhalalisha Yondani kuichezea Yanga. Rage na makamu mwenyekiti wa zamani wa Simba, Omar Gumbo ni miongoni mwa wajumbe sita wa kamati iliyotoa maamuzi ya kumruhusu Yondani kuichezea Yanga chini ya uenyekiti wa Mgongolwa, wengine wakiwa ni Hussein Mwamba na wenyeviti wa zamani wa Yanga, Lloyd Nchunga na Imani Madega.

No comments:

Post a Comment