Wednesday, September 12, 2012

POLISI ANAYEDAIWA KUMUUA KWA BOMU MWANDISHI DAUDI MWANGOSI WA CHANNEL TEN ABURUZWA KORTINI LEO... NI PC PACIFIUS CLEOPHAS SIMON... ASOMEWA MASHTAKA YA MAUAJI...!


Polisi mmoja (kushoto) akionekana kumuelekezea Daudi Mwangosi bunduki inayotumika kufyatulia mabomu.
Polisi wakimbeba mwenzao aliyejeruhiwa huku mabaki ya mwili wa Mwangosi na begi lake la laptop vikiwa chini.
Polisi anayedaiwa kuwa ndiye aliyekuwa akihaha kumuokoa Daudi Mwangosi asiadhibiwe na wenzake akiwa hoi pembeni ya mwili wa marehemu baada ya kujeruhiwa pia kwa bomu. Hapa ni kabla polisi wenzake hawajambeba na kumuwahisha hospitali.

Jeneza la mwili wa marehemu Mwangosi likipelekwa makaburini kabla ya mazishi yake yaliyofanyika Septemba 4, 2012.
Mke wa marehemu Mwangosi, Itika akilia kwa ucungu pembeni ya kaburi la marehemu mumewe.
Waandishi wa habari wakiandamana jana jijini Dar es Salaam kulaani mauaji ya mwenzao Daudi Mwwangosi. Hapa ni wakati wakitembea kutoka studio za kituo cha televisheni cha Channel Ten kuelekea viwanja vya Jangwani.
Waandishi wa habari wakiandamana jana jijini Dar es Salaam kulaani mauaji ya mwenzao Daudi Mwwangosi.
Marehemu Daudi Mwangosi (kulia) akiwapiga picha wafuasi wa Chadema dakika chache kabla ya kuuawa kwa bomu.
Marehemu Daudi Mwangosi (mwenye begi jeusi na kamera) na waandishi wa habari wenzake wakimhoji Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda muda mfupi kabla mwandishi huyo hajauawa kinyama kwa bomu.
Hapa ni siku moja kabla ya kifo chake... Daudi Mwangosi akiongoza kikao cha klabu ya waandishi wa habari wa Iringa. Yeye alikuwa Mwenyekiti wao.
HATIMAYE yule askari Polisi anayedaiwa kufyatua bomu lililomuua kinyama mwandishi Daudi Mwangosi wa kituo cha televisheni cha Channel Ten, PC Pacificus Cleophace Simon (23) amefikishwa mahakamani leo na kusomewa mashtaka ya mauaji.

Askari huyo alifikishwa mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mkoa wa Iringa, Lymo na kusomewa mashtaka hayo ya kumuua Mwangosi Septemba 2 mwaka huu.

Mwendesha Mashtaka, Michael Lwena, aliiambia mahakama kuwa upelelezi kuhusiana na tukio hilo bado unaendelea.

Mshtakiwa PC Simon hakutakiwa kujibu lolote kwani mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza mashauri ya mauaji. Hakimu Lymo aliiahirisha kesi hiyo hadi Septemba 26 mwaka huu.

Wakati akiingizwa na kutolewa kwenye viwanja vya mahakama, mshitakiwa Simon alikuwa akilindwa vikali na polisi wenzake ambapo kundi la askari zaidi ya saba walimzingira na kuzuia asipigwe picha na waandishi wa habari.

Marehemu Mwangosi aliuawa kwa bomu Septemba 2 wakati akiripoti tukio la polisi kuwazuia wafuasi wa Chadema waliodaiwa kuandamana kinyume cha sheria kwenye  tukio la ufunguzi wa tawi la chama chao kijiji cha Nyololo wilayani Mufindi mkoani Iringa.

Mlipuko wa bomu katika tukio lililomuua Mwangosi ulidaiwa pia kumjeruhi vibaya askari polisi anayetajwa kwa jina la Aceli Mwampamba.

Jana, wahariri na waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari jijini Dar es Salaam waliandamana kulaani mauaji ya Polisi dhidi ya mwenzao, Mwangosi.

Maandamano hayo yalifanyika kuanzia katika kituo cha Channel Ten na kumalizikia kwenye viwanja vya Jangwani jijini Dar es Salaam. Katika maandamano hayo ya waandishi, Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Emmanuel Nchimbi,  alilazimika kuondoka baada ya waandishi 'kumtimua' kwa kudai kwamba hawajamualika.

No comments:

Post a Comment