Wednesday, September 26, 2012

MESUT OZIL: STORI ZINAZODAI NINAJIRUSHA USIKU NI UONGO MTUPU!

Mesut Ozil
MADRID, Hispania
Nyota wa Real Madrid, amekanusha vikali madai kwamba tabia yake ya kujirusha katika viwanja vya usiku jijini Madrid inaathiri kiwango chake na kusema kwamba huo ni uzushi mkubwa dhidi yake.

Taarifa zilidai leo kwamba kocha Jose Mourinho wa Real Madrid ameingiwa hofu kutokana na tabia za nje ya uwanja za kiungo huyo mwenye miaka 23 , huku kipindi cha Futboleros kinachorushwa na kituo cha televisheni nchini Hispania kikidai kwamba tabia za mchezaji huyo nje ya uwanja zimekuwa zikimsababishia matatizo kwa zaidi ya miezi 12 iliyopita.

Hata hivyo, kiungo huyo mchezeshaji amejibu mapigo kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Facebook leo hiihii kukanusha tuhuma hizo, akisisitiza kwamba hakuna ukweli wowote kuhusiana na stori hizo.

"Kuhusiana na uvumi kwamba huwa ninajirusha kila mara usiku: Si kweli! Tangu msimu mpya uanze, sijawahi kutoka usiku. Ninafanya mazoezi na kujituma kadri ninavyoweza kwa kutambua kuwa soka ni kazi yangu," aliandika.

Ozil alichangia kwa kiasi kikubwa mafanikio ya Real Madrid iliyotwaa ubingwa wa La Liga, Ligi Kuu ya Hispania msimu uliopita, lakini kumekuwa na uvumi kuhusiana na hatma yake klabuni hapo kufuatia ujio wa Luka Modric kwenye klabu hiyo katika kipindi kilichopita cha usajili wa majira ya kiangazi.

Ameshacheza mara nane msimu huu katika kikosi cha mabingwa hao wa Hispania.

No comments:

Post a Comment