Friday, September 21, 2012
MANCINI AKANUSHA KUGOMBANA NA BALOTELLI KUELEKEA MECHI YAO YA JUMAPILI DHIDI YA ARSENAL
KOCHA wa Manchester City, Roberto Mancini amekanusha ripoti kwamba amegombana na straika Mario Balotelli kuelekea mechi yao ya Ligi Kuu ya England Jumapili dhidi ya Arsenal.
Straika huyo mwenye umri wa miaka 21 aliachwa nje ya kikosi kilicholala 3-2 dhidi ya Real Madrid katika Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya Jumanne usiku na kuchochea uvumi kwamba amegombana na meneja wake.
Lakini, Mancini amekanusha uvumi huo, akidai kwamba ilikuwa ni suala la kubadilisha kikosi tu na kwamba straika huyo wa Italia atakuwa fiti kuikabili Arsenal.
"Huu ni uongo mtupu," Mancini aliiambia Sky Sports.
"Mario alikaa jukwaani kwa sababu tulimchezesha Carlos Tevez na huwezi kuwa na mastraika watatu kwenye benchi.
"Hapakuwa na majibizano, na hakuna ugomvi wowote. Hata kidogo."
Wakati kocha huyo mwenye umri wa miaka 47 alithibitisha kwamba Samir Nasri yuko shakani kuikabili klabu yake ya zamani, baada ya Mfaransa huyo kutoka katika mechi ya Jumanne kutokana na majeraha ya misuli ya nyuma ya paja.
Majeraha ya kiungo huyo Mfaransa si makubwa kama yalivyofikiriwa awali, lakini Mancini amesema hatarajiwi kurejea Jumapili.
"Sidhani kama atakuwa tayari kucheza Jumapili," Mancini aliongeza. "Tutajaribu lakini ni ngumu.
"Nadhani atakuwa tayari kwa wiki ijayo."
Labels:
Michezo
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment