Kocha wa Yanga, Tom Saintfiet siku alipowasili jijini Dar es Salaam Jumatano Julai 4, 2012 na kupokewa kwa mbwembwe. |
YANGA imemtimua kocha wake Mbelgiji Tom Saintfiet baada ya kuitumikia klabu hiyo kwa siku 80 kamili.
Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya klabu ya Yanga, Abdallah Ahmad Bin Kleb, amethibitisha kufukuzwa kwa Mbelgiji huyo ambaye ameiongoza Yanga katika mechi 14, kushinda 11, vipigo viwili na sare 1.
Saintfiet aliyetua nchini Jumatano, Julai 4, 2012, amefukuzwa siku moja tu baada ya kuwatuhumu wachezaji kuwa "masharobaro" kama moja ya sababu za mwanzo mbaya wa msimu kwa timu hiyo ambayo inashika nafasi ya 13 katika msimamo wa timu 14 za Ligi Kuu ya Tanzania Bara ikiwa na pointi 1 kutokana na mechi mbili - sare ya 0-0 dhidi ya Prisons Jumamosi na kipigo cha aibu ambacho hakikutarajiwa cha 3-0 ugenini dhidi ya Mtibwa Sugar ya Morogoro.
Kabla ya kuwatuhumu wachezaji kwa kujiona mastaa wakubwa na kubadili mitindo ya nywele kila baada ya siku tatu ili kupamba kurasa za magazeti, Mbelgiji huyo alianika jinsi walivyolazwa wawili wawili mjini Mbeya wakati walipoenda kucheza dhidi ya Prisons katika mechi ya ufunguzi wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
Alilalamikia wachezaji kucheleweshewa chakula na wenye hoteli na kwamba alilazimika kuoga kwa kutumia kopo kutokana na mabomba ya 'mvua' ya kutotoa maji.
Hivi karibuni, Saintfiet alilalamikia kutolipwa mshahara wake wa miezi miwili, kutofurahishwa kwake na maisha ya kukaa hotelini badala ya kutafutiwa nyumba na pia kutopewa gari binafsi ya kutembelea na badala ya kuendeshwa kwenye "kipanya" cha klabu hiyo ambapo yeye amekuwa akikaa siti ya mbele.
Kipigo cha Mtibwa kimethibitisha kuichanganya timu hiyo ambayo mapema leo uongozi wake ulitangaza kuisimamisha kazi Sekretarieti nzima ya klabu, akiwamo Katibu Celestine Mwesigwa na Ofisa Habari, Louis Sendeu, "kutokana na utendaji usioridhisha".
Akizungumza na waandishi wa habari kwenye makao makuu ya klabu Jangwani jijini Dar es Salaam, Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga alisema kwamba maamuzi hayo yamefuatia kikao cha Kamati ya Utendaji kilichofanyika tangu saa 5:30 leo hadi saa 9:30.
Wengine waliosimamishwa ni Philip Chifuka aliyekuwa mhasibu, Masoud Saad, aliyekuwa Ofisa Utawala na Hafidh Saleh aliyekuwa Meneja ambaye atapewa majukumu mengine. Taarifa nyingine zimedai kuwa nyota wa zamani wa klabu hiyo Sekilojo Chambua anatarajiwa kutangazwa meneja mpya.
Sanga alisema watamtangaza meneja mwingine katika kikao kitakachofanyika klabuni hapo kesho saa 3:00 asubuhi.
Saintfiet ambaye pia alipewa onyo na uongozi kwa "kuongea ovyo na vyombo vya habari", aliiwezesha Yanga kutwaa ubingwa wa Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati maarufu Kombe la Kagame kwa mara yao ya pili mfululizo baada ya kuifundisha timu hiyo kwa kipindi cha chini ya wiki tatu.
REKODI YA SAINTFIET YANGA
1. Yanga v JKT Ruvu (kirafiki) 2-0
2. Yanga v Atletico (Burundi, Kagame) 0-2
3. Yanga v Waw Salam (Sudan, Kagame) 7-1
4. Yanga v APR (Rwanda, Kagame) 2-0
5. Yanga v Mafunzo (Z’bar, Kagame) 1-1 (5-3 penalti)
6. Yanga v APR (Rwanda, Kagame) 1-0
7. Yanga v Azam (Kagame) 2-0
8. Yanga v African Lyon (kirafiki) 4-0
9. Rayon v Yanga (kirafiki, Rwanda) 0-2
10. Polisi v Yanga (kirafiki, Rwanda) 1-2
11. Yanga v Coastal Union (kirafiki) 2-1
12. Yanga v Moro United (kirafiki) 4-0
13. Prisons v Yanga (Ligi Kuu) 0-0
14. Mtibwa v Yanga (Ligi Kuu) 0-3
No comments:
Post a Comment