Thursday, September 13, 2012

KIKAPU TAIFA WAPATA KOCHA KUTOKA MAREKANI


SHIRIKISHO na Mchezo wa Kikapu Tanzania (TBF) leo kimemtangaza, Albert Sokaitis kutoka katika Chuo Kikuu cha Post kilichoko Marekani kuwa kocha mpya wa timu ya taifa ya mchezo huo.

Sokaitis ambaye atakuja nchini pamoja na msaidizi wake, Jocquis Sconiers pia atakinoa kikosi cha timu ya taifa ya wanawake ya mchezo huo.


Akizungumza jijini Dar es Salaam leo, Makamu wa Rais wa TBF, Phares Magesa, alisema kuwa makocha hao watawasili nchini Septemba 21 mwaka huu na siku inayofuata wataanza rasmi kazi ya kufundisha hapa nchini.


Magesa alisema kuwa jukumu la kwanza la makosa hayo itakuwa ni kuziongoza vyema timu za Tanzania katika mashindano ya Ukanda wa Tano yatakayofanyika hapa nchini mwezi Desemba mwaka huu kwa kushirikisha timu za nchi 12 za Afrika.


Alisema kwamba lengo la kumleta kocha huyo mwenye uzoefu wa kufundisha mchezo huo kwa miaka 24 ni kuinua kiwango cha mpira wa kikapu nchini na atakapokuwa hana mashindano atatoa mafunzo wa makocha wazalendo wa klabu mbalimbali za hapa nchini.


"Tunaushukuru ubalozi wa Marekani hapa nchini ndio umefanikisha kutoa tiketi za makocha hao na malazi yao wakati TBF tukiendelea na mazungumzo na serikali kwa ajili ya kutekeleza ahadi yake ya kugharamia makocha wageni," alisema Magesa.


Aliongeza kuwa TBF imejipanga kuona timu zake zinafanikiwa kufuzu tiketi ya kushiriki mashindano ya kimataifa yajayo ikiwamo ya Afrika na Olimpiki.


Alisema kwamba endapo mipango na mazungumzo yatakwenda vizuri wanatarajia kukaa na makocha hao kwa muda wa miaka minne ili waweze kutekeleza programu za kuinua viwango vya wachezaji chipukizi.

No comments:

Post a Comment