Thursday, September 13, 2012

ZAWADI ZA ROCK CITY MARATHON 2012 ZATAJWA


WAANDAJI wa mbio za mwaka huu za Rock City Marathon, kampuni ya Capital Plus International (CPI), imetangaza maboresho ya zawadi zitakazoshindaniwa katika tamasha hilo litakalofanyika Oktoba 28, mwaka huu katika uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

Akitangaza zawadi hizo jijini Dar es Salaam leo, mratibu wa mbio hizo, Grace Sanga, alisema kuwa vinara wa mbio za kilomita 21 kwa upande wa wanaume na wanawake, watajishindia Sh. milioni 1.2, mshindi wa pili ataondoka na Sh. 900,000 huku mshindi wa tatu akizawadiwa Sh. 700,000.

 "Maboresho ya zawadi yamefanyika katika mbio zote kutokana na kupata udhamini mzuri kutoka Shirika la Hifadhi la Taifa (NSSF), Airtel, Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), African Barrick Gold, Nyanza Bottlers, Parastal Pensions Fund (PPF), Geita Gold Mine, Tanapa, Sahara Communications, ATCL, New Mwanza Hotel na New Africa Hotel,” alisema Sanga.

Mbio za mwaka huu zenye kauli mbiu ‘tukuze utalii wa ndani kupitia michezo’, zitahusisha washiriki wa kutoka nchi jirani, ambao mbali na kushindana na wanariadha wa ndani, wanapata fursa ya kutembelea baadhi ya vivutio vya kitalii vinavyopatikana jijini Mwanza kama vile kisiwa cha Saa Nane, miamba inayocheza iliyopo Ukerewe pamoja na kuliona Ziwa Victoria, hatua ambayo itasaidia kutangaza utalii wa Tanzania.

Alisema kwa washiriki watakaoshika nafasi kuanzia ya nne mpaka ya 10, watazawadiwa Sh. 150,000 wakati wale watakaoshika nafasi kuanzia ya 11 mpaka 25, watajipatia Sh. 100,000 katika mbio za kilomita 21 kwa wanaume na wanawake.

 “Mbio nyinginezo zinazojumuisha washiriki wote, kama mbio za kilomita tano, vinara watajishindia Sh. 50,000 kila mmoja, mshindi wa pili atapata sH. 30,000 na wa tatu ataondoka na Sh. 20,000 wakati watakaoangukia katika nafasi ya nne mpaka 25, wataondoka na Sh. 15,000 kila mmoja,” alisema Sanga.

Aliongeza kuwa kwa mbio za kilomita tatu zitakazohusisha wazee na walemavu, kinara atapata Sh. 50,000, mshindi wa pili ataondoka na Sh. 30,000 na mshindi wa tatu ataweka kibindoni Sh. 20,000 wakati kwa watakaoshika nafasi ya nne mpaka 25, wataondoka na Sh. 15,000 kila mmoja.

Kwa mbio za kilomita mbili zitakazohusisha watoto kuanzia umri wa miaka saba mpaka 10, mshindi ataondoka na Sh. 30,000, wa pili atapata Sh. 20,000 na wa tatu atapata Sh. 15,000, wakati watakaoshika nafasi kuanzia ya nne mpaka ya 25, watajinyakulia Sh. 10,000 kila mmoja.

Mwaka jana, vinara katika mbio za kilomita 21 walizawadiwa Shilingi milioni moja kwa wanaume na wanawake, mshindi wa pili aliondoka na Sh. 700,000 wakati mshindi wa tatu alijinyakulia kitita cha Sh. 500,000.

No comments:

Post a Comment