Sunday, September 9, 2012

DAVID VILLA AFURAHI KUREJEA NA GOLI TAIFA HISPANIA IKIUA SAUDI ARABIA

David Villa wa timu ya taifa ya Hispania akishangilia goli lake wakati wa mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya Saudi Arabia kwenye Uwanja wa Municipal de Pasaron juzi Ijumaa usiku Septemba 7, 2012. Hispania ilishinda 5-0.
David Villa akiwa uwanjani

 STRAIKA wa Barcelona, David Villa amefurahishwa na kurejea kwenye timu ya taifa baada ya goli lake kwa Hispania kuchangia ushindi wa 5-0 katika mechi ya kirafiki dhidi ya Saudi Arabia.

Villa, ambaye ndio kwanza anarejea uwanjani baada ya kuvunjika mguu Desemba na kukosa kampeni za Hispania za kutetea kimafanikio ubingwa wao wa Ulaya, alifunga penalti ya dakika ya 63 katika ushindi huo muda mfupi baada ya kuingia kuchukua nafasi ya Fernando Torres.

Straika huyo anayeongoza kwa kuifungia timu ya taifa ya Hispania mabao mengi zaidi katika historia, alisema: "Hakika ni siku muhimu kuweza kurejea kwenye timu ya taifa baada ya kwa nje kwa muda mrefu, ni jambo kubwa kwangu, hasa kurejea katika kikosi chenye wachezaji wenzangu, kwa sababu nimewamiss kote mazoezini na kwenye mechi.

"Hakuna sababu ya kuangalia nyuma sasa na naweza kuangalia mbele na kufurahia maisha tena."


Hispania walitawala mechi hiyo tangu mwanzo huku Saudi Arabia wanaofundishwa na kocha wa zamani wa Barcelona, Frank Rijkaard walifanya mashambulizi mara chache.

Mabingwa wa dunia ambao hawakucheza mechi ya kuwania kufuzu kwa fainali za dunia za 2014, hata hivyo walikumbana na wakati mgumu kuupita ukuta uliojaa walinzi katika kipindi cha kwanza. Hata hivyo, kwa faida ya ufundi na vipaji binafsi magoli yalikuwa yakisubiri muda tu kuja.

Kiungo wa Arsenal, Santi Cazorla alifungua sherehe za timu yake kumfunga kipa Waleed Abdullah katika dakika ya 22. Dakika sita baadaye Pedro akapiga la pili. Mwanzoni mwa kipindi cha pili, 'fri-kiki' ya Xavi ikatinga wavuni licha ya kwamba mpira kudunda ndani na kurudi uwanjani.

Vicente del Bosque akawaingiza wachezaji kama David Villa, Iker Casillas, David Silva na Andres Iniesta katika kipindi cha pili na kuzidi kuwapa ugumu Saudi Arabia "kufufuka" katika mechi hiyo.

Villa aliyerejea kwa mara ya kwanza kikosini baada ya kupona majeraha ya muda mrefu, alifunga goli kutokana na penalti iliyofuatia madhambi aliyochezwa Sergio Ramos katika eneo la hatari.

Miamba hao wa dunia wakakamilisha ushindi mnono kwa goli jingine kutoka kwa Pedro. Straika huyo wa Barca alifunga goli lake la pili katika mechi hiyo katika dakika ya 73 baada ya kupokea pasi kutoka kwa Silva.

Wakati Pedro alicheza kwa kiwango cha juu, Fernando Torres ambaye alicheza mechi yake ya 100 kwa timu ya taifa alikosa nafasi mbili za wazi katika kipindi cha kwanza na alitoka bila ya goli katika mechi ambayo kiwango cha wenzake kilimfichia makosa.

No comments:

Post a Comment