kAKA |
Beki wa Barcelona, Dani Alves ameishambulia Real Madrid kutokana na kile anachodai kuwa ni kumpuuza Kaka, huku akiongeza kwamba Mbrazili mwenzake huyo angethaminiwa zaidi kama angekuwa katika klabu ya Barcelona.
Kaka ambaye ni Mwanasoka Bora wa Dunia wa zamani amekuwa akihaha kupata namba katika kikosi cha kwanza cha Real Madrid na pia kuambulia nafasi ya kucheza tangu alipojiunga na klabu hiyo mwaka 2009, hasa baada ya kuumia.
Kaka mwenye miaka 30 alikuwa akihusishwa na uhamisho wa kurejea katika klabu yake ya zamani ya AC Milan wakati wa kipindi kilichomalizika hivi karibuni cha dirisha la usajili wa majira ya kiangazi, na Alves anasema kwamba Kaka alipaswa kuachana na Real Madrid.
"Kama ningekuwa Kaka, tayari ningekuwa nimeshahama Real Madrid," beki huyo wa kulia amesema katika mahojiano yake na Esporte Interactivo.
Ameendelea kueleza, "Kwa sababu katika maisha yangu napenda sana kucheza soka, na kama utaninyang'anya kitu hicho ninachokipenda, nitakosa raha ya maisha. Najisikia vibaya kwa sababu namkubali sana Kaka na nisingependa kukutana na masaibu yanayomtokea sasa.
"Amefikia kiwango ambacho ni wachache sana hukifikia -- cha kuwa mwanasoka bora wa mwaka wa dunia, na sasa haheshimiwi hata na wamiliki wao. Nadhani asingekumbana na hali hii kama angekuwa Barcelona."
Beki huyo mwenye miaka 29 alieleza vilevile namna anavyomzimia kocha wao wa zamani, Pep Guardiola, aliyeiacha Barcelona na kupumzika kwa muda.
"Guardiola ndiye kocha bora zaidi niliyewahi kukutana naye, aliyekamilika zaidi, mtu ambaye kila siku unajifunza kitu kutoka kwake," amesema Alves.
"Hiyo ndio tofauti yake na makocha wengine. Anasema: 'niaminini na tutashinda mechi'. Kwahiyo namkubali kwa sababu ni kocha anayeweza kukushawishi kwamba yeye ndiye njia ya ushindi."
No comments:
Post a Comment