Tuesday, August 14, 2012

YAYA TOURE: MAN CITY TUMESHAMSAMEHE CARLOS TEVEZ... ATATUSAIDIA KUTETEA UBINGWA WA LIGI KUU YA ENGLAND KWA VILE NI STRAIKA ANAYETISHA...!

Yaya Toure na Carlos Tevez wakishangilia bao walilofunga katika mechi mojawapo ya Ligi Kuu ya England msimu uliopita.

Carlos Tevez na Yaya Toure wakiwa na Kombe la FA walilotwaa Mei 23, 2011.

Nipishe hukooo...! Carlos Tevez wa Manr City (kulia) akimtoka David Luiz wa Chelsea wakati wa mechi yao ya kuwania Ngao ya Jamii kwenye Uwanja wa Villa Park mjini Birmingham, Jumapili iliyopita.
Tunatishaaaaaa....! Carlos Tevez (kulia) na Yaya Toure (kushoto) wakishangilia baada ya kuifunga Chelsea na kutwaa Ngao ya Jamii Jumapili iliyopita. Aliyeinyanyua Ngao hiyo ni nahodha wao Vincent Kompany. Wengine ni straika Sergio Aguero (wa pili kushoto).
MANCHESTER, England
KIUNGO wa Manchester City, Yaya Toure anaamini kwamba kurejea kwa Carlos Tevez kutaisaidia sana klabu yao kutimiza lengo lakle la kutetea ubingwa wa Ligi Kuu ya England, na kufichua zaidi kuwa straika huyo amesamehewa na kila mmoja baada ya kuomba radhi kwa timu nzima kutokana na vitendo vya utovu wa nidhamu alivyoonyesha msimu uliopita .


Straika huyo wa kimataifa wa Argentina alifunga bao zuri wakati Man City ikitwaa Ngao ya Jamii kutokana na ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Chelsea na hivyo kujiongezea heshima aliyo nayo klabuni hapo baada ya kuonyesha kiwango cha juu pia katika mechi chache za mwisho wa msimu uliopita akitokea kuwa nje ya timu hiyo kwa miezi sita.

Yaya ambaye ni kiungo wa zamani wa Barcelona, amempongeza Tevez, na kusema kwamba anaamini klabu yao imeshaachana na mambo ya msimu uliopita na sasa inaangalia namna ya kuzidi kusonga mbele.

“Carlos siku zote amekuwa akijitolea sana kwa ajili ya klabu,” Toure aliwaambia waandishi wa habari. 


“Mara zote amekuwa na msaada mkubwa katika kile ambacho hadi sasa tayari tumeshakifanya. Alifanya makosa, lakini kitu muhimu zaidi baada ya kukosea ni kuomba radhi. Naye ameshamuomba radhi kila mtu. Amerejea na anataka kuonyesha kwamba yuko tayari kufanya kila analoweza kwa ajili ya timu. Kwangu mimi, kitu muhimu kuliko vyote ni kujitolea kwake kwa sababu kijana huyu anatisha.

"Ni miongoni mwa wachezaji muhimu zaidi kikosini na tunafurahi kuwa naye kwa sababu ni mchezaji mzuri sana. Ni mchezaji safi anayejua wajibu wake na siku zote amekuwa akijifua sana. Carlos ni miongoni mwa wachezaji bora. Mlishuhudia (dhidi ya Chelsea) namna mara zote alivyokuwa hatari sana kwa mabeki wao. 


Wote hawa, yeye na (Sergio) Aguero ni mapacha wanaoendana vizuri. Wamewahi kucheza pamoja katika timu ya taifa ya Argentina na sasa wanaichezea Manchester City. Nina uhakika kwamba watafunga magoli mengi kwa ajili ya klabu.”

Kocha wa Man City, Roberto Mancini ameunga mkono kauli ya Yaya, akiongeza kwamba anaamini Tevez amerudisha tena mapenzi yake kwa mchezo wa soka baada ya tukio la kukataa kuingia uwanjani kucheza katika mechi yao ya Ligi ya Klabu Nigwa Ulaya dhidi ya Bayern Munich Septemba iliyopita.

“Nimefurahi kwa sababu mwaka huu Carlos amefanya vizuri sana katika maandalizi ya msimu na kiwango chake kimekuwa bora zaidi,” alisema Mancini. 


"Vilevile, mwaka huu anataka kucheza soka. Kwa mchezaji, hali huwa ngumu wakati asipocheza. Msimu uliopita, Carlos hakucheza kwa miezi sita na hali hiyo ni ngumu."

“Kwahiyo natarajia awe mchezaji muhimu sana msimu huu. Msimu uliopita tulikuwa na Carlos katika mechi 10 za mwisho na alikuwa mchezaji muhimu kwa sababu alifunga kati ya mabao tano au sita. Lakini hakuwa sawa kwa asilimia 100. Mwaka huu ni mara ya kwanza katika miaka minne, labda mitano hivi, kumuona akishiriki maandalizi yote ya msimu na kwa kila mchezaji hili ni jambo muhimu.”

Toure alihitimisha kwa kusema kwamba Man City wanaweza kutetea taji lao la Ligi Kuu ya England wakiwa na kikosi kamili na chenye malengo -- lakini pia akikumbushia umuhimu wa kurekebisha matokeo mabaya yaliyowafanya watolewe katika hatua ya makundi ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya.

Yaya aliongeza: “Jambo muhimu zaidi kwetu ni kuendelea kuimarika. Wakati timu inapotumia fedha, haitumii tu kwa sababu ya kujifurahisha. Mnapaswa kuendelea kuwa na wachezaji wazuri ili kuwa na kikosi kikali na chenye ushindani."

“Kwahiyo kuna watu wengi wanaotuongelea. Tunajua itakuwa kazi ngumu kurejea mafanikio ya msimu uliopita. Tulicheza vizuri msimu mzima na msimu huu utakuwa wa kuvutia zaidi. Kama nisingeamini kuwa nitabeba kombe lolote nikiwa Man City, ningekuwa tayari nimeshaondoka."

“Tunataka kuipeleka mbali timu hii kadri itakavyowezekana. Ni muhimu sana kwa klabu hii kufuzu kwa hatua ya pili ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya. Tuna kikosi kizuri sana, chenye kocha bomba na hivyo ninaamini tutafika mbali.”

No comments:

Post a Comment