Thursday, August 23, 2012

WACHEZAJI ANAOVUTA BANGI, UNGA MWISHO WAO UMEFIKA - TENGA

Rais wa TFF, Leodegar Tenga (katikati mbele) akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari.

Na Mwandishi Wetu
MSIMU huu utakuwa mgumu kwa wachezaji wanaotumia dawa zinazokatazwa michezoni nchini, Rais wa Shirikisho la Soka Nchini (TFF), Leodegar Tenga, amesema.


Akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari nchini kwenye ofisi za TFF jijini Dar es Salaam, Tenga amesema kuwa wachezaji watapimwa kwa kustukiza kwa kipindi chote cha msimu katika ngazi zote za ligi hadi timu ya taifa na kwamba atakayebainika kuutumia dawa zinazokatazwa ikiwamo bangi, wataadhibiwa.
"Tutawapima kwa kustukiza, mchezaji atakayekataa kupimwa atakumbana na adhabu kali sana," alisema Tenga.


Amesema hana ushahidi lakini amesikia kwamba wachezaji wengi wanavuta bangi na kwamba wamedhamiria kukomesha jambo hilo katika mchezo wa soka nchini.


"Tutaanza kwa kutoa elimu. Tutawafahamisha vijana madhara ya kutumia dawa hizi, kisha tutaanza kuwapima kwa kuwastukiza. Atakayekamatwa atapewa adhabu kali," amesema.


Aidha, Tenga alisema wanatarajia utaratibu wa tiketi za umeme uanze kutumika mapema iwezekanavyo baada ya benki ya CRDB kushinda tenda ya kuanzisha ujtaratibu huo katika viwanja vya soka nchini.


"Ni jambo linalohitaji muda kiasi kwasababu wanahitaji kufunga mitambo yao uwanjani pale, hivyo wataanza na viwanja vya Dar es Salaam kisha wataelekea mikoani," amesema. 


Ameongeza kwamba wamedhamiria kuona ligi za soka zinachezwa mwaka mzima kuanzia chini kabisa katika ngazi ya wilaya, mkoa hadi taifa ili kuwajenga wachezaji kiushindani.


"Wachezaji wakubwa kama akina Lionel Messi wanacheza mechi kuanzia 60 kwa msimu wakati wachezaji wetu hapa anayecheza mechi nyingi sana labda anafikisha mechi 35 kwa msimu. Hiki ni kidogo. Nyie mnafahamu mchezaji wa kiushindani anatakiwa kucheza angalau mechi 40 kwa msimu. Ndio maana tunataka ligi zichezwe tangu ngazi za chini kwa mwaka mzima," amesema Tenga, ambaye amekataa kusema kama atagombea katika uchaguzi mkuu wa TFF Desemba mwaka huu.


"Kila mtu anajua hilo. Sitaki kusema saa hii kwasababu uchaguzi uko mbali sana. Sio sahihi kuzungumzia uchaguzi kwa sababu kila jambo linakwenda kwa kalenda na muda wa jambo hilo haujafika. Wanaofanya hivyo kama wapo, maana tunasikia wapo, wanafanya makosa makubwa kabisa. Tukianza kuzungumzia hili hatutaweza kufanya kazi. Hapa bado tuko katika mazungumzo ya mkataba mpya kwa ajili ya kuendesha ligi, bado tunatafuta mfumo wa kuendesha ligi chini ya bodi itakayosimamia, kwa hiyo tuna mambo mengi ya kufanya hivi sasa," ameongeza.


Tenga pia aliomba radhi kwa wanahabari kufuatia tukio la kughasiwa kwa waandishi wa habari katika mechi ya fainali ya Kombe la Kagame kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, lililosababisha Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo (TASWA) kutoa tamko la kuacha kuripoti chochote kinachohusu michuano hiyo ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati.


"Nikiwa kama Rais wa CECAFA na TFF naomba radhi kwa kilichotokea kwa sababu hakukuwa na sababu ya kutokea. Tutahakikisha tunaweka mikakati ili yasitokee tena," amesema Tenga.



No comments:

Post a Comment