Tuesday, August 7, 2012

VAN PERSIE ARUDI ARSENAL, KUANZA KUJIFUA NA KINA LUCAS PODOLSKI, OLIVIER GIROUD, SANTI CARZOLA….!


Van Persie
Santi Carzola... mmoja wa nyota wapya wa Arsenal wanaodaiwa kumvutia Van Persie na kumfanya afikirie mara mbili uamuzi wake wa kutaka kuondoka.
Lucas Podolski... mkali mwingine aliyesajiliwa na Wenger hivi karibuni.
Nuri Sahin.... kiungo huyu nyota anatarajiwa kutua Arsenal kutoka Real Madrid. Inaelezwa kuwa ujio wake pia unamshawishi Van Persie kutaka kubaki Arsenal.
LONDON, England
NAHODHA wa Arsenal, Robin van Persie ameungana na wachezaji wenzake wa klabu ya Arsenal kwenda Ujerumani kujifua kwa ajili ya msimu ujao huku hatma yake katika klabu hiyo bado ikiwa njiapanda.


Straika huyo, ambaye alishatangaza dhamira yake ya kutaka kuondoka Arsenal katika barua ya wazi aliyowaandikia mashabiki wa klabu hiyo mwezi uliopita, alikwea pipa na wachezaji wenzake na pia kocha Arsene Wenger jana na kwenda Ujerumani wanakotarajiwa kucheza mechi ya kirafiki dhidi ya Koln mwishoni mwa wiki.

Mholanzi huyo amezivutia klabu za Juventus, Manchester City na Manchester United baada ya kuhoji hadharani malengo ya klabu hiyo Julai 4, kufuatia Arsenal kumaliza msimu wa saba mfululizo bila kutwaa taji lolote, na pia msimu uliopita kumaliza ikiwa nyuma ya Man City na Man U kwa pointi 19.

Hata hivyo, imebainika kwamba Van Persie amefurahishwa na usajili wa nyota kutoka Malaga, Santi Cazorla na pia jitihada za kumleta kiungo Nuri Sahin kutoka Real Madrid, hivyo anaelekea kubadili uamuzi wake wa kutaka kuhama na badala yake kuungana na wenzake katika mazoezi ya kujiandaa na msimu.

Olivier Giroud na Lukas Podolski, ambaye anaweza kucheza dhidi ya timu yake ya zamani katika mechi ya kirafiki ya Jumapili kwenye Uwanja wa RheinEnergie, tayari walishasajiliwa na Wenger wakati wa dirisha la usajili unaoendelea wa majira ya kiangazi.

No comments:

Post a Comment