Tuesday, August 7, 2012

FAO LA KUJITOA: SERIKALI YAKUBALI YAISHE, WAZIRI ALIAMBIA BUNGE JIONI HII KUWA INAKWENDA KUFUTILIA MBALI KIPENGELE KINACHOZUIA FAO LA KUJITOA


Waziri wa Kazi na Ajira, Mhe. Gaudentia Kabaka
Serikali imewaondoa hofu wafanyakazi nchini kote kuhusiana na utata juu ya fao la kujitoa baada ya kutangaza rasmi jioni hii kwamba inakwenda kukifutilia mbali kipengele kinachowazuia kuchukua fao hilo.

Waziri wa Kazi na Ajira, Mhe. Gaudentia Kabaka, ameyasema hayo bungeni jioni hii wakati akijibu swali lililotaka kujua msimamo wa serikali juu ya agizo la hivi karibuni lililotolewa na Mamlaka ya Mifuko ya Hifadhi (SSRA) kuwa kuanzia Julai 20, 2012, hakuna mfanyakazi atakayeruhusiwa kuchukua fao la kujitoa kwa maelezo kwamba sheria iliyopitishwa na Bunge April, 2012 inazuia jambo hilo.

Waziri Kabaka alitakiwa pia kutoa kauli ya serikali kuhusiana na taarifa kwamba wafanyakazi wa migodini wamegoma kwa sababu ya kupinga kipengele hicho cha “kinyonyaji” cha sheria ya SSRA kinachozuia wafanyakazi kulipwa fao la kujitoa.

Akijibu swali hilo wakati bunge lilipokaa kama kamati kupitia vifungu vya bajeti ya wizara yake jioni hii, Mhe. Kabaka akawataka wafanyakazi wa migodini na kwingineko nchini kuwa na subira kwani sheria hiyo itafanyiwa marekebisho na kuletwa tena katika kikao kijacho cha Bunge ili kuondoa kipengele kinacholalamikiwa.

“Nawasihi wafanyakazi wa migodini wawe na subira na kuendelea na kazi kwa amani… ni kwa sababu kikao kijacho si mbali sana, nadhani ni Novemba… au mwezi mmoja na nusu hivi ujao… kipengele hicho kitafanyiwa marekebisho,” alisema Waziri Kabaka na kushangiliwa na wabunge.

Hivi karibuni, Mkurugenzi wa SSRA, Irene Isaka alizua mtafaruku na taharuki kubwa miongoni mwa wafanyakazi nchini (hasa vijana) baada ya kutoa tangazo la kuzuia uchukuaji wa fao la kujitoa hadi watakapotimiza miaka 55 na 60, akidai kwamba kufanya hivyo ni kwenda kinyume na sheria ya mifuko ya hifadhi iliyopitishwa na bunge April.

Wafanyakazi wengi, kupitia vyama vyao mbalimbali walikuja juu na kupinga vikali sheria hiyo kwa kusema kwamba ni ya “kinyonyaji” kwani wastani wa umri wa kuishi kwa Watanzania uko chini ya miaka 55 na pia, kazi nyingi siku hizi ni za mikataba na hivyo wengi hawana uhakika wa kuendelea na ajira zao hadi kufikia umri huo.

Kuona hivyo, wabunge nao wakaja juu. Mbunge wa Kisarawe, Mhe. Suleiman Jaffu, akawasilisha jana hoja ya kutaka sheria iliyounda SSRA ipitiwe upya na kuondoa kipengele kinachozuia wafanyakazi kuchukua ‘fao la kujitoa’.

No comments:

Post a Comment