Sunday, August 12, 2012

TANZANIA OLIMPIKI SASA BAAAAAASI...! NI BAADA YA WANARIADHA WAKE KUANGUKIA PUA MARATHON LEO KWA KUMALIZA KATIKA NAFASI ZA 33 NA 66, WENZAO UGANDA, KENYA WAGAWANA MEDALI ZA DHAHABU, FEDHA NA SHABA

Mtanipenda tu... Mganda Stephen Kiprotich akishangilia wakati akimaliza katika nafasi ya kwanza leo kwenye mbio za marathon za michezo ya Olimpiki jijini London 2012.

Hebu wacheki hawa jamaa.... katika kundi hili la wakali waliokuwa wakimfukuzia Mganda Kiprotich kuna Mtanzania kweli?  Ila wote hawa walichemka na Kiprotich akatwaa medali ya dhahabu ya mbio za marathon za Olimpiki jijini London leo.

Wakimbiaji waliokuwa wakiwania medali ya dhahabu ya Olimpiki kwa mbio za marathon leo walikuwa wengi... lakini Kiprotich akaibuka kinara, Wabongo watatu wakabaki kuwa wasindikizaji!

Hapa ndipo mahala palipoanzia mbio za marathon leo na kumaliziwa.... Mganda Kiprotich akakomba maujiko kwa kutwaa medali ya dhahabu. Kama kawa, Watanzania wakaambulia medali "sifuri"!
Wanamichezo wa Tanzania walioshiriki Olimpiki ya London 2012... hapa ni wakikaribia kukwea 'pipa' kwenye Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere kabla ya kuelekea jijini London.
Tanzania imejihakikishia kutwaa medali "0" katika michezo inayomalizika leo ya Olimpiki jijini London 2012 baada ya wakimbiaji wake Faustine Mussa, Samson Ramadhani na Mohamed Msenduki kuangukia pua katika mbio ndefu za marathon ambazo medali zake zote zimetwaliwa na Uganda na Kenya.

Faustine Mussa alishika nafasi ya 33 na nahodha wa timu hiyo ya riadha ya Tanzania, Samson Ramadhani, alikamata nafasi ya 66, hivyo kuendeleza rekodi ya kusikitisha ya Tanzania ya kupeleka washiriki wanaorudi mikono mitupu katika michezo hiyo tangu miaka ya 1980.

Kabla ya leo, washiriki wengine miongoni mwa Watanzania saba waliopelekwa katika mashindano hayo walishatolewa mapema na kubaki kuwa kama "watalii" jijini London, wakiwa ni pamoja na bondia Selemani Kidunda aliyedundwa vibaya wakati akichapwa kwa pointi 20-7, mwanariadha Zakia Mrisho aliyekamata nafasi ya 31 kati ya wakimbiaji 36 na kutolewa mapema katika mbio za wanawake za mita 5,000 huku pia waogeleaji wawili wakishindwa kufurukuta, akiwamo Magdalena Moshi.

Katika mbio za leo za marathon, Mganda Stephen Kiprotich (23) aliwashangaza Wakenya na kutwaa medali ya dhahabu huku medali za fedha na shaba zikiangukia kwa Wakenya Abel Kirui na Wilson Kipsang. 


Kiprotich alimuacha Kirui kwa sekunde 26, na hiyo ilikuwa ni medali ya kwanza ya dhahabu kwa taifa la Uganda katika michezo ya Olimpiki baada ya kupita miaka 40.

Miaka ya 1980 ilikuwa ndio ya mwisho kwa wanamichezo wa Tanzania kuambulia medali katika michezo ya kimataifa kupitia kwa wanariadha Filbert Bayi ambaye sasa ndiye bosi wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) na Suleiman Nyambui, ambaye pia hivi sasa anashikilia nafasi ya katibu wa Riadha Tanzania (RT).

No comments:

Post a Comment