Sunday, August 12, 2012

DK. ULIMBOKA ATUA NCHINI NA KUPOKELEWA KWA MASHADA YA MAUA, AKWEPA KUFUNGUKA ZAIDI KUHUSIANA NA WATU WALIOMTEKA, KUMTESA NA KUMTUPA KWENYE MSITU WA MABWE PANDE AKIWA HOI ...!Dk. Ulimboka (wa pili kushoto) akipokewa na kwa mashada ya maua baada ya kutua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam leo. 
Dk Ulimboka alivyokuwa wakati akiendelea kutibiwa.
Dk. Ulimboka alivyokuwa kabla ya kukutwa na mkasa wa kutekwa, kuteswa na kutupwa kwenye msitu wa Mabwepande
Kiongozi wa Jumuiya Madaktari nchini, Dk. Steven Ulimboka amerejea nchini leo saa 1:55 mchana akitokea Afrika Kusini na kupokewa na mamia ya watu kabla ya kutoa kauli yenye matumaini kwa wote wanaomuunga mkono kwa kusema kuwa sasa anajisikia mzima wa afya.

Akizungumza kwa ufupi SANA ikiwa ni muda mfupi tu baada ya kutua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam na kupokewa na mamia ya watu, Dk. Ulimboka alisema amefurahi kurejea nyumbani akiwa salama, na kwamba sasa "yuko fiti" kufanya kazi yoyote atakayopangiwa.

“Naona afya yangu imeimarika… namshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa hatua hii niliyoifikia. 

“Ningependa kuwashukuru ndugu, kuwashukuru jamaa na kuwashukuru marafiki. Ningependa kuwashukuru madaktari kwa kufanikisha safari hii na ninawahakikishia kwamba nimepona, niko fiti na ninaweza kufanya jambo lolote lile,” alisema Dk. Ulimboka.

Dk. Ulimboka alitoa shukrani zake kwa madaktari wenzake, asasi za kiraia, wanaharakati mbalimbali na wananchi wa kawaida waliojitokeza kumchangia pesa za kumpeleka Afrika Kusini ambako hatimaye alipata matibabu mazuri na kupona kabisa.

Hata hivyo, daktari huyo aliyekuwa mstari wa mbele kupigania maslahi ya madaktari wakati wakiendesha mgomo wao wa nchi nzima kutetea maslahi yao hivi karibuni, hakuzungumzia kabisa undani wa matibabu yake na wala kugusia tena mkasa wa tukio lake la kutekwa, kupewa mateso makali na kutupwa kwenye msitu wa Mabwepande uliopo nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.

Baada ya kutua kwenye Uwanja wa Ndege jijini Dar es Salaam,  Dk. Ulimboka alilakiwa na wapendwa wake kwa shangwe, vigelegele na mashada ya maua; kama ilivyo kwa shujaa yeyote yule anaporejea kutoka mahala alikofanya tukio kubwa na la kihistoria.

Madaktari wenzake ndio waliokuwa wengi na mstari wa mbele kumpa Dk. Ulimboka mapokezi hayo ya kishujaa, wakishirikiana na ndugu, jamaa na marafiki mbalimbali. Baadhi ya wanaharakati waliokuwepo uwanjani hapo ni pamoja na watokao Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) na Mtandao wa Kijinsia Tanzania (TGNP).

Mabango kadhaa yenye ujumbe mbalimbali yalitumika wakati wa kumpokea Dk. Ulimboka.

Akizungumza uwanjani hapo, Katibu Mkuu wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk. Edwin Chitage, alisema kuwa kamwe hawataacha kupigania maslahi yao.

Ananilea Nkya kutoka TAMWA alisema kuwa wanaharakati hawatasita kuendelea kupigania maslahi ya madaktari na wananchi wengine nchini.   

Tukio la kutekwa kwa Dk. Ulimboka wakati madaktari wakiwa kwenye mgomo lilizua gumzo kubwa nchini, huku gazeti lililofungiwa baadaye la Mwanahalisi likiandika kwa kina juu ya tuhuma zilizoenea dhidi ya baadhi ya maafisa wa Usalama wa Taifa kuwa walihusika katika kumteka na kumfanyia unyama wote aliokumbana nao.

Hata hivyo, Idara ya Usalama wa Taifa ilikanusha tuhuma hizo na kuziita kuwa ni za 'uzushi'.  Kwa zaidi ya mara moja, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Jakaya Kikwete alikanusha pia juu ya madai kwamba serikali imehusika na utekwaji wa Dk. Ulimboka na kusisitiza kwamba hakuna sababu yoyote kwa serikali yake kumdhuru Dk. Ulimboka.

Aidha, Kamanda wa Polisi katika Kanada Maalum wa Dar es Salaam, Suleiman Kova, alitoa taarifa za kukamatwa kwa raia wa Kenya aitwaye Joshua Mhindi kuhusiana na tukio la kutekwa kwa Dk. Ulimboka.

Kamanda Kova alieleza kuwa mtuhumiwa alitiwa mbaroni baada ya kwenda kuungama makosa yake kwenye kanisa la Ufufuo na Uzima lililopo Kawe jijini Dar es Salaam na kukiri kwamba ndiye aliyetekeleza mpango huo wa utekaji akishirikiana na wenzake wa kundi la Gun Star.

Hata hivyo, Mchungaji Josephat Gwejima wa kanisa hilo alikanusha baadhi ya maelezo ya polisi kuhusiana na mtu huyo.

Aidha, wabunge kadhaa walipaza sauti zao na kutaka uchunguzi mkali ufanyike ili waliohusika na tukio hilo la "kinyama" wafikishwe mbele ya mkono wa sheria.

Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi 'Mr. II - Sugu' alieleza hofu yake kuhusiana na maelezo ya polisi na kufikia hatua ya kumtaka Kamanda Kova arejee studio kutokana na kile alichodai kuwa "filamu yake na mchungaji haikueleweka".

No comments:

Post a Comment